Joseph Kabila, rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), amekuwa kwenye majukwaa ya siasa kwa zaidi ya robo karne, lakini sasa jina lake linafungamanishwa na hukumu ya kifo aliyopewa bila kuwepo. Hukumu hiyo imefungua ukurasa mpya wa safari yake yenye mchanganyiko wa mafanikio, lawama na siri nyingi.

Kabila, mwenye umri wa miaka 54, alihukumiwa na mahakama ya kijeshi kwa kosa la usaliti na kuhusiana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda. Serikali inadai alishirikiana nao kutikisa utawala wa Rais Felix Tshisekedi.

Safari yake ya kisiasa ilianza mwaka 2001, baada ya baba yake Laurent-Désiré Kabila kuuawa na mlinzi wake binafsi. Akiwa kijana mwenye sauti ya taratibu, wengi walimwona kama kiongozi dhaifu, lakini alidumu madarakani hadi mwaka 2019.

Katika kipindi chake cha uongozi, Kabila aliongoza taifa tajiri kwa rasilimali lakini lenye mizozo mikubwa. Aliwahi kusifiwa kwa kusimamia uchaguzi wa kwanza huru tangu uhuru mwaka 2006, lakini pia alikumbwa na lawama za kukandamiza upinzani na rushwa.

Baada ya kung’atuka, alihama nchi mwaka 2023 na kujikita zaidi Afrika Kusini na Namibia. Hata hivyo, kurejea kwake Goma mwezi Mei mwaka huu, eneo linalodhibitiwa na M23, kuliamsha hofu kubwa mjini Kinshasa.

Hapo ndipo serikali iliposukuma ajenda ya kuondolewa kinga yake ya ubunge wa maisha na kuanzisha kesi ya uhaini, hatimaye kumpelekea hukumu ya kifo bila kuwepo mahakamani.

Kongo Kinshasa | Joseph Kabila na Felix Tshisekedi
Félix Tshisekedi (kulia) akipokea skafu ya urais kutoka kwa Joseph Kabila baada ya kula kiapo kama Rais wa Kongo, Januari 24, 2019.Picha: Jerome Delay/dpa/picture alliance

Kutoka nje ya mfumo hadi Ikulu ya Kinshasa

Joseph Kabila alizaliwa tarehe 4 Juni 1971 katika ngome ya baba yake huko Kivu Kusini. Utoto wake mwingi aliutumia uhamishoni Tanzania, kabla ya kurejea 1996 wakati wa Vita ya Kwanza ya Kongo.

Baadaye alipata mafunzo ya kijeshi nchini China na akajiunga na jeshi la Kongo mwaka 1998 wakati Vita ya Pili ya Kongo ilipoanza. Mwaka 2001, alipoingia madarakani, taifa lilikuwa limegawanyika na serikali kuu ikidhibiti sehemu ndogo tu ya nchi.

Kutokana na malezi yake uhamishoni na ukosefu wa ufasaha wa Kifaransa na Lingala, lugha inayotumika Kinshasa, alionekana mgeni katika mji mkuu. Lakini alikuwa na nguvu zaidi mashariki mwa Kongo, ambako alipewa jina la “mtu wa mashariki.”

Kabila mara nyingi alionekana mwenye aibu hadharani, akipendelea shughuli za vitendo kama kuendesha matrekta. Rafiki zake walimwelezea kama mtu msiri, mwenye nidhamu na anayeipenda faragha.

Hata hivyo, aliwashangaza wanadiplomasia wa kigeni kwa ustadi wake wa kisiasa, akivunja dhana kwamba alikuwa tu kikaragosi cha wakongwe wa utawala wa baba yake. Uchaguzi wa 2006 ulimthibitisha rasmi kama rais, na ulikuwa wa kwanza huru tangu uhuru.

Nigeria | Rais Obasanjo (katikati), akiwa na Rais wa Rwanda Kagame (kushoto)
Rais wa Nigeria wakati huo Olusegun Obasanjo (katikati), akiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame (kushoto), na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila katika jengo la kifalme la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nnamdi Azikiwe mjini Abuja, tarehe 25 Juni 2004.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP

Kutoka mafanikio hadi lawama na anguko

Mwaka 2011, aliwania muhula wa pili na kushinda kwa kura zilizokumbwa na tuhuma za wizi na kasoro kubwa. Upinzani ulipinga matokeo na maandamano makubwa yakazuka, na kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Mnamo 2015, jaribio lake la kuwania muhula wa tatu liliibua maandamano makubwa zaidi. Shinikizo la ndani na la kimataifa lilimlazimisha hatimaye kung’atuka, na kutoa nafasi ya kwanza kwa mabadiliko ya kidemokrasia tangu uhuru wa nchi hiyo.

Kabla ya kuondoka, alituhumiwa kupanga kumpa Tshisekedi ushindi kupitia makubaliano ya kisiasa yaliyolenga kuendelea kuwa na ushawishi nyuma ya pazia. Hata hivyo, ushirikiano huo ulivunjika ndani ya miaka miwili tu.

Kabila, katika mahojiano machache aliyoyafanya, amejitambulisha kama kiongozi wa kawaida aliyejitahidi kulijenga taifa lililoharibiwa na vita. Alikanusha madai ya kutoa mikataba ya madini kwa wageni kwa hasara ya maendeleo ya taifa.

Kama Mkristo wa Anglikana, Kabila amemuoa Marie Olive Lembe Kabila na wana watoto wawili, Sifa na Laurent-Désiré. Maisha yake ya kifamilia yalibaki siri kubwa, yakilingana na hulka yake ya kujitenga.

Lakini sasa, akiwa amepoteza nguvu za kisiasa na akikabiliana hukumu ya kifo, Kabila yupo katika ncha ya safari yake yenye misukosuko, akisubiri mustakabali wake uamuliwe na historia na siasa za DRC.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *