
“Uhamiaji ni uhalisia wa wakati wetu, hasa kwa vijana,” amesema Ugochi Daniels, Naibu Mkurugenzi wa Operesheni wa IOM. “IOM inaunga mkono Wakawell Youth Hackathon kwa sababu inatoa nafasi kwa vijana kubuni na tunajua kuwa zana za kidijitali wanazounda ni muhimu katika kufanya sera za uhamiaji kuwa za kisasa na zenye kujibu mahitaji yao halisi.”
Tukio hilo la siku mbili limewaleta pamoja washiriki 20 kutoka Cameroon, Ethiopia, Kenya, Liberia, Mali, Nigeria, Tanzania na Uganda, walioteuliwa kutoka kwa zaidi ya waombaji 200. Wakishirikiana na washauri kutoka IOM, walitengeneza kikundi cha mtandao wa kijamii kwa kutumia Akili Mnemba (AI) ili kuimarisha jukwaa la Wakawell Youth Hackathon. Jukwaa hili linatoa taarifa sahihi kuhusu uhamiaji kwa vijana wa Kiafrika wanaotaka kusoma, kufanya kazi au kushiriki michezo barani Afrika.
Tangu lilipozinduliwa miaka 5 iliyopita, WakaWell Youth Hackathon limekuwa chanzo cha kuaminika kwa vijana wanaojiandaa na safari za uhamiaji. Mwaka 2024, zaidi ya watu 62,000 walitumia jukwaa hilo, ambalo kwa sasa linahudumia nchi nane za Afrika Magharibi na Kaskazini. Upanuzi kuelekea Afrika Mashariki umepangwa mwaka huu, ili kufikia jumla ya nchi 11.
“Hackathon imeonesha nguvu ya mtazamo wa Panafrika, Uhamiaji unaweza kuwa ushindi kwa pande zote mbili kwa nchi zinazohitaji vipaji na kwa vijana wa Kiafrika wanaotafuta fursa za kazi na elimu.” amesema mjumbe wa jukwaa hili Ciku Kimeria, ambaye pia ni mwandishi wa habari kutoka Kenya.