Kupitia video iliyochapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto Kanda ya Afrika, Angelique Kidjo anakumbuka safari yake ya kujifunza, kuanzia kuchora herufi za kwanza nyumbani hadi kugundua furaha ya kusoma. Anakumbuka jinsi baba yake alivyochochea udadisi wake kwa kumpa daftari, jambo lililomfanya apende kuandika.
“Nadhani nilianza kusoma na kuandika nyumbani na kaka zangu. Baba alinunua daftari. Nikaaanza kuandika kwa sababu tu ilikuwa inanivutia kuona herufi A inavyoonekana kubwa na ndogo. Nakumbuka maneno mawili ya kwanza niliyoandika yalikuwa mama na baba. Kisha yakafuata namba moja hadi kumi. Nilipofika kumi nikasema, wow. Baba akaniambia, hapana, huo ndiyo mwanzo tu,”
Kwake, kujifunza kuligeuzwa kuwa jambo la kufurahisha, jambo analoamini ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto.

Balozi wa Mwema wa UNICEF Angelique Kidjo akishirikiana na watoto katika makazi yasiyo rasmi ya Housh el Refka, katika Bonde la Bekaa nchini Lebanon.
Mwanamuziki huyo kutoka nchini Benin, Magharibi mwa Afrika anasisitiza wajibu wa wazazi katika kukuza fikra za watoto akisema, “ninaamini kabisa katika wazazi kutafuta muda wa kuwasomea watoto wao na kusoma nao. Inafungua udadisi. Mtoto akipouliza swali, usimwambie tu, ondoka. Tunapaswa kulisha ubongo na roho,” anasema, akiongeza kwamba ushirikiano huo hujenga uhusiano wa kudumu na kukuza elimu ya maisha yote.
Ingawa anakiri kwamba aliwahi kupata ugumu katika hisabati, Kidjo anamsifu mwalimu wake mwenye ari aliyemsaidia kushinda changamoto hiyo.
“Kilichonivutia nilipokuwa mdogo nikijifunza mambo yote hayo ni kwamba walinifanya nione ni kama mchezo. Sarufi na msamiati vilikuwa ninavyovipenda zaidi. Kujifunza lugha yoyote na kuweza kuiandika kwa usahihi ilikuwa muhimu sana kwangu. Lakini sikuwahi kupenda hisabati. Nilikuwa na mwalimu wa hesabu. Aliingia darasani akaanza kuandika mambo haya. Kisha akasema, ‘Nitaeleza kwenu maana ya hesabu. Ni mantiki tu.’ Nikasema, oh, hili ni jambo la kufurahisha. Kwa mara ya kwanza nikapata alama nzuri kwenye hesabu kwa sababu ya ari ya mwalimu huyo. Hiyo ilinirudisha kwenye misingi ambayo nilikuwa nimeiacha kando.”

Balozi Mwema wa UNICEF na mshindi wa Tuzo za Grammy Angélique Kidjo akitumbuiza kwenye maadhimisho ya Umoja wa Mataifa ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake mwaka 2020. (Maktaba)
Sasa UNICEF inaziomba serikali za Afrika kufanya uamuzi wa “uwekezaji wa busara” utakayohakikisha kila mtoto anapata ujuzi wa msingi wa kujifunza. Kwa mujibu wa shirika hilo, kuwekeza katika elimu bora hakutabadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja pekee bali pia kutaleta mustakabali wenye nguvu na mafanikio kwa bara zima. Kidjo ameunga mkono wito huo, akionya kwamba bila uwekezaji thabiti katika kizazi kijacho, Afrika itapoteza nafasi yake ya kufikia uwezo wake kamili.
Anasema, “Tunapaswa kuelimishwa ili kuelewa ugumu na upeo wa bara letu, ili tuweze kuelewa ugumu wa dunia. Tukishindwa kufanya hivyo kwa kizazi kijacho, tayari tunapoteza mengi.”