
Ripoti ya hali ya Ebola iliyotolewa na WHO ikiishia kipindi cha Jumanne Septemba 30 inaonesha kuna wagonjwa wapya 7 ambapo kati yao, 6 wamethibitishwa kuwa na Ebola.
Idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na wagonjwa wapya 11 walioripotiwa kwenye ripotiya awali ya tarehe 21 mwezi uliopita wa Septemba.
Mlipuko wa Ebola ulitangazwa rasmi Kasai tarehe 15 mwezi Septemba na umejikita katika kanda sita za kiafya ambazo ni Bambalae, Bulape, kata ya Bulape, Dikolo, Ingongo na Mpianga.
Lakini kwa sasa maeneo ambako wameripotiwa wagonjwa wapya ni kanda ya kiafya ya Bulape ambayo ni Bulape Mpianga na Dikolo .
Vifo miongoni mwa watoto wenye umri wa siku 0
Katika kipindi husika vifo saba vimeripotiwa miongoni mwa wagonjwa wapya na wale wa zamani.
Tangu kuripotiwa kwa mlipuko jumla ya washukiwa 64 wa Ebola waliripotiwa na kati ya 53 walithibitishwa. Kati yao waliokufa ni 42 ambapo 31 walikufa kwa Ebola na miongoni mwao ni wahudumu wa afya 5.
Kwa upande wa umri, WHO inasema wanaokufa wana umri wa kuanzia miaka 0 yaani watoto wachanga waliozaliwa hadi watu wenye umri wa miaka 65.
Kati ya wanawake na wanaume, WHO inasema idadi ya wagonjwa wengi ni wanawake, halikadhalika idadi ya wanaokufa.
Mapema Jumanne akihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, Bintou Keita alieleza kuwa mlipuko wa Ebola huko Kasai, umeongeza janga la kibinadamu.