Katika ujumbe wake kwa Siku ya Kimataifa ya Wazee mwaka huu wa 2025, Katibu Mkuu wa UN António Guterres amebainisha mabadiliko makubwa ya kidemografia, akieleza kuwa idadi ya watu walio na zaidi ya umri wa miaka 60 imeongezeka mara mbili katika miongo mitatu iliyopita, na kufikia bilioni 1.2.
Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa kufikia mwaka 2050, watu wengine milioni 900 zaidi wanatarajiwa kujiunga na Kundi hilo kote duniani.
Kuwawezesha wazee ni kipaumbele cha maisha
“Wazee ni washirika wenye nguvu ya mabadiliko,” amesema Guterres akiongeza kuwa “Sauti zao lazima zisikike katika kuunda sera, kukomesha ubaguzi wa rika, na kujenga jamii jumuishi.”
Amesisitiza kwamba jamii lazima zichukue hatua kwa busara ili kuhakikisha haki na heshima za wazee zinalindwa na zinaheshimiwa kikamilifu, huku zikitambua mchango wao usio na kifani kwa jamii kote duniani.
Hekima kati ya vizazi
Katibu Mkuu amebainisha kuwa jamii zote zinafaidika na hekima ya wazee, akitanabaisha uwezo wao wa kipekee wa kushughulikia hali zisizo na uhakika, kutatua migogoro, na kujenga mshikamano kati ya vizazi.
“Tuzingatie ahadi ya kusikiliza, kujifunza, na kuchukua hatua” amesema Katibu Mkuu akisisitiza kuwa “Tujenge dunia ambayo kila mtu wa kila umri anaweza kuishi kwa heshima, usalama, na fursa.”
Kaulimbiu ya hatua na utetezi
Siku ya Kimataifa ya Wazee 2025 inaadhimishwa chini ya kaulimbiu “Wazee Wanaendesha Hatua za Kijamii na Kimaisha: Matamanio Yetu, Ustawi Wetu na Haki Zetu.”
Kaulimbiu hii inaangazia nafasi ya mabadiliko wazee wanayoweza kuleta katika nyanja kama usawa wa afya, ustawi wa kifedha, uimara wa jamii, na utetezi wa haki za binadamu.
Umoja wa Mataifa unasema Wazee hawapo kama wapokeaji tu, bali wanatambuliwa kama waendeshaji wa maendeleo katika ngazi za kijamii na kimataifa.

Candelario anafurahia kusoma na kuwa na mazungumzo mazuri.
Kukamilika kwa sera za kimataifa
Maadhimisho ya mwaka huu yanajengwa juu ya mifumo ya muda mrefu, ikiwemo Mpango wa Kimataifa wa Madrid wa Hatua za Uzee (MIPAA) ulioidhinishwa mwaka 2002.
Guterres amebainisha kuwa maendeleo ya hivi karibuni, kama azimio la Baraza la Haki za Binadamu la Aprili 2025, nambari 58/13, la kuunda chombo cha kisheria kinacholinda haki za wazee, yanaonesha kutambuliwa kwa uwepo wa wazee kama wamiliki wa haki na wachechemuzi wa mabadiliko.
Mabadiliko ya kidemografia yanahitaji hatua za haraka
Kwa kuwa wazee wanawakilisha sehemu inayoongezeka kwa haraka ya jamii, hasa katika nchi zinazoendelea, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa upatikanaji wa haki sawa wa huduma za afya, ulinzi wa kijamii, na sera za kupinga ubaguzi ni muhimu kwa maendeleo endelevu.
Siku ya Kimataifa ya Wazee 2025 inatumika kama jukwaa kwa wazee kuzungumza kuhusu matamanio yao, kutetea haki zao, na kuomba sera zinazohakikisha heshima na ustawi wao.