
Akihutubia wakati wa kufunga mjadala huo, Bi Baerbock kutoka Ujerumani, amesema ‘Umoja wa Mataifa ni nyumba ya diplomasia na mazungumzo, akisifu ushiriki imara wa mataifa 189 kati ya 193 wanachama, ambapo kati ya hizo 83 ziliwakilishwa na wakuu wa nchi ilhali 41 wakuu wa serikali.
Umuhimu wa Umoja wa Mataifa
“Umoja wa Mataifa bado una umuhimu mkubwa hasa wakati huu wa njia panda, migogoro ya dunia ikiendelea kuongezeka,” amesema Rais huyo wa UNGA80.
Baerbock amesisitiza kuwa uwakilishi una maana, akitaja mfano wa kihistoria wa viongozi wanawake 9 waliotoa hotuba zao siku ya Jumatatu katika maadhimisho ya miaka 30 tangu Azimio la Beijing.
Amekumbusha wanachama kuwa, “Iwapo wanawake si huru, hatimaye hakuna atakayekuwa huru,” na kwamba usawa wa kijinsia si suala la maadili tu bali pia ni la kiuchumi, kwa uwezo wa kuongeza hadi dola trilioni 7 kwenye uchumi wa dunia.
Mwelekeo baada ya Mjadala Mkuu UNGA80
Kuhusu njia ya kusonga mbele, Baerbock amewasihi wajumbe kupeleka msukumo huo wanaporejea kwenye nchi zao, na kuunga mkono juhudi za mageuzi ya Umoja wa Mataifa.
Kuanzia hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na ujenzi wa amani hadi usimamizi wa teknolojia ya akili mnemba na usawa wa kifedha, amesisitiza umuhimu wa majawabu ya pamoja kwa changamoto za kimataifa, akithibitisha kuwa hakuna nchi inayoweza kukabiliana nazo peke yake.
“Nguvu tuliyoihisi wiki hii lazima igeuke kuwa vitendo,” amehitimisha akisema, “tuchukue ujasiri wa kuunda mustakabali bora—kwa pamoja.”