Balozi Bizimana amesisitiza historia ya Umoja wa Mataifa katika kuendeleza amani na ushirikiano tangu kuanzishwa kwake mwaka 1945. “Leo, tunaposherehekea kumbukumbu hii, nina heshima ya kuthibitisha dhamira ya Burundi kwa misingi ya awali iliyoendesha Umoja wa Mataifa kwa miaka 80,” amesema.

Amepongeza pia mada ya kikao hiki cha mwaka huu, “Kwa pamoja tu Bora Zaidi: Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu,” akiielezea kama “kibali cha maadili na njia muhimu kuelekea mustakabali wa pamoja.”

Safari ya Burundi kutoka migogoro hadi amani

Waziri huyo amesema, “Burundi ni mfano hai wa ustahimilivu na amani iliyorejea. Taifa letu limepitia nyakati ngumu sana, lakini kupitia na kwa sababu ya nia ya wananchi wake na taasisi zake zilizoboreshwa, imeweza kufunga ukurasa wa migogoro na kuchagua njia ya maridhiano, utulivu, na heshima ya pande zote.”

Amesema Bizimana akielezea kazi ya Tume ya Ukweli na Maridhiano na uchaguzi wa hivi karibuni wa bunge na halmashauri za mitaa kama hatua za kuonesha ukomavu wa kidemokrasia wa taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika.

Bizimana pia amekosoa michakato yenye upendeleo inayoilenga Burundi na nchi nyingine. “Tunapinga mifumo maalumu inayowekewa baadhi ya nchi, ikiwemo Burundi, kwa sababu zisizo za msingi,” alisema. Ameutaka pia Umoja wa Mataifa kuondoa dhamana ya Mwakilishi Maalumu wa Haki za Binadamu kwa Burundi, akirejelea miaka 10 ya ripoti alizoziita za “zenye upendeleo na za kugeuza ukweli.” Licha ya changamoto hizi, amethibitisha ahadi ya Burundi kwa haki za binadamu, majadiliano na ushirikiano.

Wito wa marekebisho UN na uwawakilishi wa Afrika

Waziri pia ameutaka Umoja wa Mataifa kufanya marekebisho ya haraka, akisisitiza usawa na ujumuishi. “Amani na haki za binadamu haviwezi kustawi bila haki za kijamii na usawa miongoni mwa mataifa,” amesema.

Amebainisha kwamba Afrika kukosa kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama ni dhuluma ya kihistoria inayohitaji kurekebishwa. “Hii si fadhila ni haki kamili ikiwa Umoja wa Mataifa unataka kubaki thabiti kwa misingi yake,” amesisitiza Bizimana.

Kujenga mustakabali wa pamoja

Akihitisha hotubba yake waziri huyo wa Burundi amesema nchi yake inathibitisha ahadi yake ya kuchangia kikamilifu katika amani, maendeleo endelevu, na mshikamano. “Ndiyo, kwa pamoja tu bora zaidi, na ndipo tunaweza kulinda amani, kuhakikisha haki za binadamu, na kuimarisha mustakabali wa heshima kwa watoto wetu,” meeleza Bizimana.

Ametoa wito kwa nchi zote wanachama kuungana katika ushirikiano wa kimataifa ulio jumuishi, unaoendana na haki, na unaohakikisha Umoja wa Mataifa unakabiliana na changamoto za dunia ya sasa na kusikiliza sauti zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *