Kusimama kwa shughuli za serikali ya Marekani ina maana kwamba baadhi ya huduma za serikali hiyo zitakwama kwa muda na mishahara ya maelfu ya wafanyakazi wa serikali itasimamishwa.
Hali hiyo imejitokeza baada ya wabunge wa chama cha Republican na wale wa chama cha Democrats kushindwa kufikia makubaliano juu ya mswada wa matumizi ya fedha za serikali.
Wabunge wa chama cha Democatic siku ya Jumanne jioni walilikwamisha azimio lililopendekezwa na wenzao wa chama cha Republican lililolenga kuipa serikali muda wa kuendelea na shuguli zake. Hatua hiyo haikupata uungwaji mkono wa kutosha na hivyo kukosa kufikia kura 60 zilizohitajika ili kupitishwa.
Trump atishia kutumia matokeo kuwanyima ajira wafanyakazi wa serikali
Sababu kuu iliyosababisha hali hiyo ya mkwamo wa bajeti ni juu ya fedha za matumizi kwa ajili ya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na kuendeleza ufadhili ambao ulipitishwa kisheria wa huduma ya afya ya bei nafuu maarufu kama Obamacare. Seneta Chuck Schumer, Kiongozi wa Wachache bungeni wa chama cha Democratic amesema wasiwasi wake na chama chake ni kuhusu afya ya Wamarekani na kwamba hatua walioichukua ni sahihi na inawawakilisha wapiga kura wao.
Rais Donald Trump, ametishia kutumia matokeo hayo ya kusimama kwa shughuli za serikali yake kuwaachisha kazi kwa wingi wafanyikazi wa serikali.
Sarafu ya Marekani Dola, imeporomoka na kwenda chini dhidi ya sarafu zingine kuu hii leo Jumatano huku idaara zikionya kuwa kufungwa kwa shughuli za serikali kutasimamisha pia kutolewa ripoti kuhusu ajira iliyofuatiliwa kwa karibu katika mwezi uliomalizika wa Septemba na kuna hofu ya kusimamishwa kazi kwa wafanyikazi wa serikali wapatao 750,000 ambao gharama ya malipo yao ni dola milioni 400 kwa siku.
Hii ni mara ya kwanza ya kufungwa kwa shughuli za serikali ya Marekani katika muda wa takriban miaka saba. Mara ya mwisho shughuli za serikali ya Marekani kukwama ilikuwa mwishoni mwa mwaka 2018 hadi mapema 2019 katika wa muhula wa kwanza wa Donald Trump wakati wademocratic na chama cha Trump cha Republican walijikuta kwenye mvutano pale Trump alipotaka ziidhinishwe zaidi ya dola bilioni 5.7 kwa ajili ya kujenga ukuta ili kuwazuia wahamiaji kuingia Marekani.