Chanzo cha picha, CCM
-
- Author, Na Charles William
- Nafasi, Mchambuzi
Ni wazi kwamba joto la kisiasa nchini Tanzania sasa limepanda kwenye kiwango cha juu kabisa. Vyama vyote vyenye ushawishi mkubwa kwa wananchi tayari vimetangaza wazi mikakati yake na kuanza kutambulisha wagombea wao kuelekea uchaguzi ambao kampeni zake zinatarajiwa kuanza mwezi Julai na kutamatika Oktoba 2025.
Januari 19, 2025 Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndio chama tawala kinachoendesha serikali nchini Tanzania kiliazimia na kumthibitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wake wa Urais, lakini pia kimemteua na kumthibisha Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea wake katika nafasi ya Makamu wa Rais.
Kwa upande wa Urais wa Zanzibar, sehemu ya pili ya Muungano wa Tanzania chama hicho kilitangaza kumteua Rais wa sasa, Dk. Hussein Mwinyi kuwa mgombea wake kwa asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Maamuzi ya mapema
Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania
Hatua ya CCM kufanya uteuzi wa wagombea wake mwezi Januari, haikutarajiwa na wengi na wala haikuwa sehemu ya ajenda zilizotangazwa katika ratiba rasmi ya mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika kwa siku mbili mfululizo, Januari 18 na Januari 19 jijini Dodoma. Kwa kawaida chama hicho huteua wagombea wake kati ya mwezi Mei mpaka Julai katika mwaka wa uchaguzi.
Rais Samia alieleza kwamba Makamu wa sasa wa Rais, Dk. Philip Mpango hatakuwa mgombea mwenza wake katika kinyang’anyiro cha Urais mwaka huu kwasababu yeye mwenyewe ameomba kupumzika majukumu hayo ili kujipa muda wa kutosha wa kuiangalia afya yake, ndipo akamtangaza mwanasiasa mashuhuri hapa nchini, Dk. Emmanuel Nchimbi kama mgombea mwenza wake.
Dk. Nchimbi ni mwanasiasa mwenye uzoefu mkubwa sana katika siasa za ndani ya chama tawala. Amewahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa Vijana wa chama hicho, amewahi kuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri serikalini kwa miaka 8 na amekuwa Mjumbe wa vikao vya juu kama Kamati Kuu na Halmashauri Kuu za chama tawala kwa zaidi ya miaka 20, na kwa sasa ndiye Katibu Mkuu wa CCM.
Inaelezwa kwamba uteuzi uliofanywa na CCM ulilenga zaidi kukipa utulivu chama hicho na kuzima minong’ono mbalimbali ambayo imekuwepo kwa muda mrefu kwamba wapo wana CCM wenye nia ya kumkabili Rais Samia katika nafasi yake. Kwa maamuzi haya yaliyofanyika miezi sita kabla ya muda wa ratiba ya uchaguzi mkuu kuanza, ni rasmi sasa hakuna mwanachama mwingine atakayeruhusiwa kujitokeza kugombea dhidi ya Rais Samia.
Tunaweza kusema kwa uteuzi wa Rais Samia na Dk. Nchimbi kuwa wagombea wake ni rasmi sasa CCM imetangaza rasmi ‘majenerali’ wake watakaotangulizwa mstari wa mbele katika mapambano ya kusaka dola kwa njia ya kidemokrasia kupitia kura za wananchi.
Lissu na Chadema mpya?
Kwa upande wake Chama Kikuu cha Upinzani hapa nchini, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimefanya uchaguzi wake mkuu, na kumchagua Tundu Lissu kuwa Kiongozi wake mkuu na kuhitimisha uongozi wa miongo miwili wa Freeman Mbowe aliyedumu madarakani kwa miaka 21.
Kuchaguliwa kwa Tundu Lissu kuwa kiongozi wa Chadema kunaleta ladha mpya ya kisiasa nchini Tanzania hasa kutokana na mwanasiasa huyo kujitwalia umaarufu mkubwa kwa wananchi kutokana na uwezo wake mkubwa wa kujenga hoja, kushawishi wananchi na misimamo mikali dhidi ya serikali iliyopo madarakani.
Lissu amewatangazia wanachama wa chama chake kuwa anayo mikakati mipya na mbinu mpya za kukabiliana na serikali iliyopo madarakani ili kutimiza azma ya chama hicho kushinda uchaguzi na kushika dola. Ametangaza pia kwamba ana nia ya kuwania urais wa Tanzania kupitia chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu.
Itakumbukwa kuwa Lissu ndiye alikuwa mgombea urais wa Chadema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, katika uchaguzi ambao mgombea wa chama tawala wakati huo Rais John Magufuli alitangazwa kuibuka na ushindi wa asilimia 84 ya kura zote zilizopigwa huku Lissu akishika nafasi ya pili. Vyama vya upinzani na waangalizi wa kimataifa na baadhi wa ndani waliukosoa uchaguzi huo kwamba haukuwa huru na wa haki na ulitawaliwa na ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu.
Matokeo ya uchaguzi huo ndio yalikuwa matokeo mabaya zaidi kwa upinzani tangu siasa za vyama vingi zianze hapa nchini Tanzania miaka 30 iliyoppita. Upinzani ulishuka kutoka kutoka asilimia 40 ya kura ulizopata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 hadi kufikia chini ya asilimia 16 ya kura mwaka 2020.
Tundu Lissu amekuwa mwanasiasa wa upinzani mwenye kuvutia wengi tangu alipochaguliwa kuwa Mbunge mwaka 2010 na kuchaguliwa tena mwaka 2015. Sifa yake kubwa ni kujenga hoja na kupangua hoja huku taaluma yake ya sheria ikimuongezea uwezo wa kudadavua hoja nyingi zinazohusu utawala wa kuzingatia sheria, haki za binadamu na utawala bora.
Umaarufu wake ulipaa zaidi baada ya kunusurika kifo katika tukio la kupigwa risasi zaidi ya 16 mwilini mwaka 2018. Tangu wakati huo amekua kinara wa upinzani. Kuchaguliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Chadema wiki hii kuna maana kuwa ndiye ataongoza chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kama mgombea Urais na mwenyekiti wa chama.
ACT na joto la Zanzibar
Chanzo cha picha, ACT Wazalendo
Kwa upande wa chama cha tatu kwa kuwa na uungwaji mkono mkubwa zaidi hapa nchini, ACT Wazalendo ambacho pia ndicho chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar ambako ni upande wa pili wa Muungano wa Tanzania nacho tayari kimetangaza muelekeo wake katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Othman Masoud Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taifa wa ACT Wazalendo ametangaza kuwania urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa mwaka huu.
Hii itakua ni mara ya kwanza kwa Othman kuwania urais, ambapo anatarajiwa kukabiliana na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi.
Itakuwa ni mara ya kwanza upinzani visiwani Zanzibar kuingia katika uchaguzi mkuu bila kinara wake wa muda mrefu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye alikuwa mshindani mkuu wa chama tawala tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.
Maalim Seif alifariki dunia Februari 2021 baada ya kuugua, hivyo katika uchaguzi wa mwaka huu Othman Masoud ndiye atakua tegemeo la upinzani.
Othman amefanya kazi kwa miaka minne sasa kama Makamu wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inayoundwa na CCM na ACT Wazalendo kwa pamoja, huku mkuu wa Serikali akiwa ni Rais Dk. Hussein Mwinyi. Wawili hawa wamekua na nyakati kadhaa za kusigana na kuvutana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utendaji wa serikali na sasa ni wazi kwamba watakabiliana katika uchaguzi.
Tarehe 16 Januari mwaka huu, Kiongozi wa ACT Wazalendo Dorothy Semu naye kwa upande wake alitangaza rasmi kuwania Urais wa Tanzania huku akisema nia yake kubwa kushughulikia hali mbaya ya kiuchumi na kurudisha uchumi wa kati, kupunguza gharama za maisha na kutatua changamoto ya ajira kwa vijana.
Mwaka 2025 ni mwaka unaotarajiwa kutawaliwa na matukio mengi ya kisiasa nchini Tanzania kutokana na uwepo wa uchaguzi utakaohusisha kuchaguliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Serikali ya Zanzibar, Wabunge wa majimbo 264, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Madiwani katika kata zipatazo 4,000 nchi nzima.
Charles William ni mchambuzi na mwandishi wa Habari za siasa kutoka Tanzania.
Imehaririwa na Athuman Mtulya