Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova, ameikosoa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa kwa kujiingiza katika masuala yaliyo nje ya mamlaka yake kwa kuunga mkono kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, akieleza hatua hiyo kama “mfano halisi wa kupendelea madola ya Magharibi.”

Mnamo Septemba 28, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ilitoa taarifa rasmi ikieleza kuwa orodha ya vikwazo vya Kamati ya 1737 ya Baraza la Usalama imeanza kutumika tena.

Zakharova alisisitiza kuwa Baraza la Usalama halijawahi kupitisha uamuzi wowote unaoiruhusu Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa “kutangaza maoni kuhusu masuala nyeti kama haya, ambayo yako chini ya mamlaka ya kipekee ya Baraza hilo.”

Aidha, alieleza kuwa hatua ya Sekretarieti hiyo ilifanyika katika mazingira ya kampeni pana ya kupotosha fikra za umma.

“Vyombo vikuu vya habari vya Magharibi vimeanza tena kusukuma kwa nguvu wazo la kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, ambavyo viliondolewa kwa mujibu wa Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA) kama sehemu ya utekelezaji wa Azimio la 2231,” aliongeza.

Mnamo Septemba 19, Baraza la Usalama lenye wanachama 15 lilishindwa kupitisha azimio ambalo lingezuia kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya Iran baada ya kundi la E3 linalojumuisha Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, kuanzisha utaratibu wa “snapback” na kuishutumu Tehran kwa kutotekeleza masharti ya JCPOA.

Kwa mujibu wa Zakharova, mataifa ya Magharibi yanapotosha ukweli kwa kudai kuwa kukataliwa kwa rasimu ya azimio la kuendeleza utaratibu wa kuondoa vikwazo ni sababu ya kurejesha masharti yaliyokuwa yameondolewa.

Amesikitika kuwa wawakilishi wa Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa wanatekeleza “njama za Magharibi kwa niaba ya Umoja wa Mataifa.”

Zakharova alipendekeza tukio hili lifundishwe katika vitabu vya sheria chini ya kichwa cha “ukiukaji wa sheria za kimataifa.”

Katika hitimisho lake, Zakharova alielezea hali nzima kama “njama za Magharibi na ubabe wa Magharibi, unaolenga kuharibu sheria za kimataifa na taasisi ya Umoja wa Mataifa.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *