Ujerumani inaadhimisha miaka 35 tangu zilizokuwa Ujerumani Mashariki na Magharibi zilipoungana na kuwa nchi moja tena. Hata hivyo, bado tofauti zinaonekana kati ya sehemu hizo mbili, hata miongoni mwa watu waliozaliwa baada ya muungano.
Elisabeth Kaiser alizaliwa mwaka 1987 katika mji wa Gera katika jimbo la Thuringia, wakati huo ikiwa Ujerumani Mashariki. Miaka miwili baadaye, Ukuta wa Berlin ulianguka, na tarehe 3 Oktoba 1990, iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani ikatupwa katika kapu la historia.
“Sikuwa na ufahamu wa kushuhudia kipindi cha muungano, ila simulizi za wazazi na mababu ndizo zimejenga mtazamo wangu,” anasimulia Elisabeth Kaiser katika ripoti ya mwaka iliyowasilishwa mjini Berlin siku ya maadhimisho ya muungano, ikiakisi maoni ya vijana kutoka Mashariki na Magharibi mwa Ujerumani.
Hiyo ni ripoti ya kwanza kwa mwanasiasa huyo wa chama cha SPD mwenye umri wa miaka 38, ambaye aliteuliwa kuwa Kamishna wa Ujerumani Mashariki mwezi Mei mwaka huu, baada ya serikali mpya kuingia madarakani.
Je, kizazi kipya cha Ujerumani kimekulia katika mazingira yanayofanana?
Katika ripoti yake ya hivi karibuni, kamishna huyo ambaye pia ni msomi wa sayansi ya siasa anajikita katika uzoefu wa vijana wa Ujerumani miaka 35 baada ya muungano. Kichwa cha habari cha ripoti hiyo kiko katika muundo wa swali, jambo linalodokeza tayari kuwepo kwa mgawanyiko unaojikita kwenye misingi ya Mashariki na Magharibi: Je, vijana wanakulia katika mazingira sawa?
Jibu rasmi kwa swali hilo ni ndiyo, kwa sababu hivi sasa kuna nchi moja ya Ujerumani. “Sisi watoto wa miaka ya mwisho ya 1980 hadi miaka ya 1990, ni kizazi cha kwanza kilichojumuika katika Ujerumani iliyoungana,” anasema Elisabeth Kaiser katika utangulizi wa ripoti yake ya mwaka.
Hata hivyo, kwa wale waliyozaliwa upande wa Mashariki, kwao suala hilo si la kijiografia pekee, bali pia ni jambo linaloshawishi namna mtu anavyojitambua, anasisitiza.
Utambulisho wa Ujerumani mashariki una nguvu kuliko wa magharibi
Linapohusika suala la utambulisho, vijana wengi kutoka iliyokuwa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani hawajitambui sana kama watu wa Ujerumani Magharibi, hususan wale wanaotoka kwenye pwani ya kaskazini, au wale kutoka milima ya Alps kusini mwa nchi. Hii ni tofauti na wenzao kutoka mashariki ambao mara nyingi wanajitambua kama watu wa mashariki.
Kipato kidogo, msaada mkubwa wa kijamii
Akinukuu kile kinachojulikana kama “ripoti ya uwiano,” Elisabeth Kaiser anasema kuwa katika miji midogo na vijiji, huduma za usafiri wa umma na vituo vya afya si tena za uhakika. Zaidi ya hayo, kipato cha wananchi wengi kiko chini ya wastani wa kitaifa, na hali hii inawalazimisha wengi wao kutegemea msaada wa serikali.
Kaiser anabainisha kuwa hali ya uchumi ni bora upande wa Magharibi ikilinganishwa na Mashariki. Hata hivyo, tofauti hii bado inaonekana miaka 35 baada ya muungano.
Eneo jingine linaloonyesha pengo ni muundo wa idadi ya watu. Ujerumani Mashariki ina idadi ndogo ya vijana ikilinganishwa na wastani wa taifa. Hali hii inawaathiri vijana wa upande huo hata wanapokomaa, kwani mara nyingi hawawezi kutegemea msaada kutoka kwa wazazi wao kwa kiwango kile kinachowezekana upande wa Magharibi.
Magharibi Tajiri, Mashariki Maskini
Wakati wa kuwasilisha ripoti yake ya mwaka, Elisabeth Kaiser alisisitiza kipengele kimoja muhimu:
“Hadi leo, vijana wa Mashariki wamekuwa katika hali ya kutotendewa haki kwa sababu mali hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.”
Ripoti ya Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho kwa mwaka 2024 inaweka hali hiyo wazi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ofisi za kodi katika majimbo ya Magharibi zilitoza kodi ya urithi au zawadi yenye thamani ya zaidi ya euro bilioni 106, huku Mashariki pamoja na Berlin zikiwa chini ya euro bilioni 7 pekee.
Kwa kila mtu, wastani wa mali hiyo ulikuwa karibu euro 1,600 upande wa Magharibi — karibu mara nne zaidi ya Mashariki, ambako wastani ulikuwa euro 400 pekee.
Tofauti hizi kubwa, Kaiser anasema, ndizo zinazomkera na zinahitaji kushughulikiwa. Ni kwa msingi huo anapotoa hoja kwamba mjadala kuhusu mabadiliko ya kodi ya urithi si jambo baya, bali unaweza kusaidia kupunguza pengo kubwa kati ya pande mbili za Ujerumani.
Euro 20,000 kama urithi wa msingi kwa kila mtu?
Elisabeth Kaiser anarejelea mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya Ujerumani (DIW) miaka michache iliyopita, kwamba serikali inapaswa kuwapa vijana wote watu wazima euro 20,000 kama aina ya urithi wa msingi wenye matumizi maalum.
Kwa mfano, fedha hizo zinaweza kutumika kulipia gharama za masomo, kuanzisha biashara ndogo, au kuwekeza katika mali isiyohamishika.
Shirika la kiraia “Urithi kwa Kila Mtu” linaunga mkono wazo hili likiliona kuwa na tija na linalowezekana kifedha. Kwenye tovuti yake, shirika hilo linaeleza kwamba mpango huo “unaweza kufadhiliwa kwa kodi ndogo inayotozwa kwenye urithi mkubwa.”
Kwa mujibu wa mahesabu ya shirika hilo, asilimia tano ya thamani ya urithi wa kila mwaka nchini Ujerumani inatosha kugharimia mpango huo bila kulipia gharama kubwa zaidi za ziada kwa walipa kodi wa kawaida.
Pengo la kiuchumi linazidi kupanuka
Kamishna wa Serikali ya Ujerumani kuhusu masuala ya Mashariki, Elisabeth Kaiser, anatambua kuwa mjadala kuhusu mageuzi ya kodi ya urithi ni suala nyeti ndani ya serikali ya mseto.
Katika chama chake, SPD, wapo wanaounga mkono wazo hilo, lakini upande wa vyama ndugu vya CDU/CSU, ni vigumu kupata maridhiano ya kisiasa.
Kwa hivyo, tofauti kubwa za kifedha kati ya Mashariki na Magharibi huenda zisiishe haraka, hata baada ya miaka 35 tangu kuungana kwa Ujerumani.
Tathmini ya jumla ya Elisabeth Kaiser ni mchanganyiko
Ujerumani Mashariki imepiga hatua katika nyanja nyingi: uchumi umekua, kuna mazingira hai ya biashara changa (start-ups), na imekuwa kinara katika maendeleo ya nishati mbadala.
Lakini yote hayo hayatoshi kwa muda mrefu kufidia pengo kati ya mashariki na magharibi.
Hali hiyo huenda ikazidi kuwa ngumu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wazee mashariki na uhamaji wa vijana wengi wanaokwenda magharibi.
Watu milioni mbili wameihama mashariki
Mbali na jiji kuu la Ujerumani, Berlin, eneo lililokuwa Ujerumani Mashariki limepoteza watu milioni mbili tangu kuungana kwa Ujerumani mwaka 1990 — upungufu ambao ni asilimia 16 ya wakaazi wote
Kwa sasa, majimbo matano ya mashariki yana wakazi takriban milioni 12.5.
Katika kipindi hicho hicho, idadi ya watu magharibi mwa Ujerumani imeongezeka kwa asilimia 10 hadi karibu milioni 68.