Baada ya Vita vya Pili vya Dunia mwaka 1945, Ujerumani iliyoshindwa iligawanywa na mataifa washindi – Marekani, Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Kisovyeti – katika maeneo manne ya ukaliaji. Kufikia mwaka 1949, yakazaliwa mataifa mawili: Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani (BRD) upande wa Magharibi yenye mfumo wa kidemokrasia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (DDR) upande wa Mashariki chini ya udhibiti wa Kisovyeti.
Kuanzia hapo Ujerumani ikawa imegawanyika. Wananchi wa DDR waliwekewa masharti magumu kusafiri kwenda BRD. Mipaka ya DDR ilikuwa ikilindwa kwa ulinzi mkali, na kuzunguka Berlin Magharibi, iliyokuwa sehemu ya BRD, ukajengwa Ukuta mkubwa wa Berlin kuzuia wananchi wa DDR kuondoka.
Jinsi Muungano wa Ujerumani ulivyopatikana
Wananchi wa DDR waliishi katika taifa la uangalizi bila uhuru wa kutoa maoni. Waliokosoa utawala wa kijamaa walikabiliwa na mateso au kifungo. Mwishoni mwa miaka ya 1980, wananchi walianza kuibua maandamano wakidai uhuru na demokrasia kama ilivyokuwa kwa majirani zao upande wa Magharibi.
Hali hii iliimarishwa na siasa za mageuzi za Mikhail Gorbatschov kiongozi wa Umoja wa Kisovyeti, ambaye hakutumia nguvu za kijeshi kuzima vuguvugu la mabadiliko. Mwaka 1989, maandamano ya amani katika miji ya Mashariki yalipelekea kufunguliwa kwa Ukuta wa Berlin – hatua iliyowezesha DDR na BRD kuungana tena.
Kwa nini tarehe 3 Oktoba?
Kuanguka kwa Ukuta wa Berlin mnamo tarehe 9 Novemba 1989 kulikuwa tukio kuu kuelekea muungano. Hata hivyo, tarehe hiyo haiwezi kusherehekewa kwa sababu ya kumbukumbu mbaya ya Reichspogromnacht (Usiku wa Krstalili) mnamo 9 Novemba 1938, wakati Wajerumani wa Kinazi walipoteketeza masinagogi, maduka na nyumba za Wayahudi na kuwaua au kuwakamata maelfu.
Kwa sababu hiyo, taifa liliamua kutumia 3 Oktoba 1990 – siku halisi ambayo DDR iliunganishwa rasmi na BRD – kama sikukuu ya kitaifa ya Muungano wa Ujerumani.
Sherehe za siku ya muungano
Sherehe hufanyika kwa utulivu. Hakuna milipuko mikubwa ya fataki wala barabara kujazwa rangi za taifa kila mahali. Badala yake, miji mingi huandaa hafla ndogo, siku za mlango wazi katika taasisi, na sherehe za kijamii. Kila mwaka, jimbo moja miongoni mwa majimbo 16 huandaa sherehe kuu ya kitaifa, kwa kawaida kwenye mji mkuu wa jimbo lenye urais wa Baraza la Shirikisho.
Mwaka huu, jimbo la Saarland ndiyo mwenyeji wa sherehe hizo, ambapo mjini Saarbrücken kunafanyika matukio ya burudani, sanaa, tamaduni, vyakula na mijadala ya kidemokrasia kuanzia tarehe 2 hadi 4 Oktoba. Kwa Wajerumani wengi, furaha kubwa zaidi ni kupata mapumziko ya kitaifa.
Kwa nini hakuna kumbukumbu rasmi ya muungano?
Bunge la Ujerumani (Bundestag) lilipitisha mnamo 9 Novemba 2007 mpango wa kujenga Mnara wa Uhuru na Muungano (Freiheits- und Einheitsdenkmal) mjini Berlin, mbele ya Jumba la Humboldt Forum. Mnara huo ulipangwa kuwa kikombe kikubwa cha mita 50 kinachoweza kutembelewa, kikionyesha demokrasia kwa vitendo – kikiwa kinasogea upande ambao watu wengi wanaelekea. Hata hivyo, kufikia mwaka 2025 bado haujakamilika, kutokana na migogoro kati ya makampuni yaliyopangiwa ujenzi na taasisi za serikali. Kitu kilichosimama tu hadi sasa ni msingi wa mnara.
Je, Ujerumani imeungana kikamilifu?
Licha ya jitihada za kisiasa, tafiti za maoni zinaonyesha bado kuna mgawanyiko. Utafiti wa Forsa unaonesha kwamba ni asilimia 35 tu ya Wajerumani wanaoamini kuwa Mashariki na Magharibi zimeungana kwa kiasi kikubwa.
Tofauti inaonekana wazi: Mashariki ni asilimia 23 pekee wanaosema Ujerumani ni taifa moja tangu 1990, wakati Magharibi ni asilimia 37. Kiwango cha juu zaidi cha mshikamano kilifikiwa mwaka 2019 kwa asilimia 51.
Kwa mujibu wa utafiti wa Infratest dimap, changamoto kubwa zaidi inayotajwa na wananchi (asilimia 50) ni kutokuwepo kwa usawa wa mishahara, pensheni na mali kati ya pande mbili.
Kwa ufupi, Siku ya Muungano wa Ujerumani ni kumbukumbu ya kihistoria ya kuunganishwa tena kwa taifa baada ya miongo kadhaa ya mgawanyiko, lakini pia ni siku ya kutafakari changamoto zinazobaki kati ya Mashariki na Magharibi.