Hatua ya serikali ya Israel kuwarejesha makwao wanaharakati hao imekuja muda mfupi tu baada ya meli yao ya mwisho kuzuiwa na jeshi la wanamaji la Israel. Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema tayari imewafukuza wanaharakati wanne raia wa Italia waliokuwa ndani ya msafara wa meli, na kuongeza kuwa wengine bado wako katika mchakato wa kufukuzwa.

Polisi wa Israeli walisema kuwa zaidi ya watu 470 wakiwemo wanaharakati na wandishi habari ndani ya meli hizo walikamatwa na polisi, wakafanyiwa uchunguzi mkali, na kisha kuhamishiwa kwa idara ya magereza.

Msafara wa Global Sumud Flotilla ulianza safari mwezi uliopita, ukiwasafirisha wanasiasa na wanaharakati wakiwemo Greta Thunberg kutoka Sweden, kuelekea Gaza ambako Umoja wa Mataifa unasema njaa kali imeanza kushika kasi.

Hakuna mahali salama kwa Wapalestina

Umoja wa Mataifa umesema kuwa hakuna mahali salama kwa Wapalestina waliokimbia mji mkuu wa Ukanda wa Gaza. 

James Elder msemaji wa shirika la watoto la Umoja wa Mataifa ameyaita maeneo ya usalama yaliyotajwa na Israel kusini mwa Gaza kuwa ni “maeneo ya kifo.”

“Mabomu yanarushwa kutoka angani kwa utaratibu wa kutisha. Shule zilizotajwa kuwa makazi ya muda zinageuzwa kuwa magofu mara kwa mara. Mahema yanashambuliwa katika maeneo hayo, na bila shaka hayatoi ulinzi dhidi ya vipande vya mabomu, na kwa kweli, kama tulivyoona, mahema hayo hayo huungua moto mara kwa mara kutokana na mashambulizi ya anga”, alisema Elder. 

Maandamano ya kuunga mkono msafara wa misaada

Mgomo na maandamno makubwa yafanyika Italia
Mgomo na maandamno makubwa yafanyika ItaliaPicha: Yara Nardi/REUTERS

Katika baadhi ya miji barani Ulaya maandamano yamefanyika kutaka usitishwaji vita huko Gaza. Waandamanaji wanaounga mkono Palestina walikaribia lango la kituo cha mazoezi cha timu ya taifa ya soka ya Italia Ijumaa (03.10.2025), wakitaka mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Israel isichezwe, Oktoba 14 ijayo, kutokana na vita vinavyoendelea Gaza.

Maandamano hayo yalikuwa sehemu ya mgomo wa kitaifa wa siku moja, uliolenga pia kushinikiza msafara wa misaada uliodhibitiwa na jeshi la Israeli. Mamia ya treni zilifutwa au kuchelewa, pamoja na ndege kadhaa za ndani, na shule nyingi za binafsi na za umma kufungwa.

Katika hatua nyingine, serikali ya Uhalonzi imetangaza kuchunguza upya usafirishaji wa vifaa vya kijeshi kwenda Israel. Kutokana na hatari ya Israel kutumia vifaa hivyo katika kampeni yake ya kijeshi huko Ukanda wa Gaza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *