
Wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Al Shabab wametekeleza shambulio jipya la kigaidi siku ya Jumamosi, Oktoba 4 huko Mogadishu, nchini Somalia. Shambulio hilo lililenga gereza la Godka Jilacow lenye ulinzi mkali, katikati mwa mji mkuu, Mogadishu. Gereza hili linasimamiwa na idara ya Ujasusi na usalama, ambayo makao yake makuu yanapatikana mita chache na gerza hilo. Vikosi vya usalama vya Somalia vinalielezea kama shambulio baya zaidi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Shambulio hilo lilitokea alasiri ya tarehe 4 Oktoba wakati gari lililokuwa na vilipuzi na kupambwa kwa rangi za idara za usalama liliendeshwa kwa kasi kuelekea gereza lenye ulinzi mkali huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, kulingana na televisheni ya taifa.
Mlipuko huo ulikuwa mkubwa sana. Kwenye mtandao wa kijamii wa X, Dk. Abdulkhadir Adan, kiongozi wa mtandao wa magari ya wagonjwa ya Aamin, alirusha picha ya video baada ya shambulio hilo, anaripoti mwandishi wetu mjini Nairobi, Gaƫlle Laleix. Safu ya moshi mweusi inaonekana, na wakazi wakimbia kwa hofu kubwa. Vyombo vya usalama vya Somalia vilidai haraka kuwa viliua washambuliaji kadhaa. Mapigano ya risasi, hata hivyo, yalichukua saa kadhaa.
Katika taarifa kwenye mtandao wake wa kijamii, kundi la Al Shabab limedai kuhusika na shambulizi hilo na kueleza kuwa wapiganaji wake wamefanikiwa kuingia katika eneo la jela. Mamlaka ya Somalia bado haijatoa idadi ya vifo. Haijabainika pia iwapo kuna wafungwa walioweza kutoroka kutoka katika gereza hilo.
Shambulizi hili lilitokea saa chache baada ya Waziri Mkuu kuzindua kampeni ya “Salama Mogadishu”. Baadhi ya barabara zaidi ya hamsini katika mji mkuu, zilizofungwa kwa sababu za kiusalama, zilikuwa zimefunguliwa tena asubuhi.
Somalia, nchi maskini na isiyo na utulivu katika Pembe ya Afrika, inakumbwa na mashambulizi mapya ya Al Shabab, kundi ambalo wanamgambo wake wanahusishwa na Al-Qaeda. Waasi hao wamechukua udhibiti wa makumi ya miji na vijiji tangu kuanza mashambulizi yao mapema mwaka huu, na kufuta karibu mafanikio yote yaliyopatikana na serikali ya Somalia wakati wa operesheni yake ya kijeshi ya mwaka 2022 na 2023.
Nchi hii imekuwa ikipigana na Al Shabab tangu katikati ya miaka ya 2000. Lakini hali ya usalama imezorota sana mwaka huu. Waasi hao walidai kuhusika na mlipuko wa bomu ambao uliukosa msafara wa rais mnamo Machi 18 na kurusha makombora kadhaa karibu na uwanja wa ndege wa Mogadishu mapema mwezi Aprili.
Shambulio la bomu la kujitoa muhanga lililenga chuo cha kijeshi kusini mwa mji mkuu wa Somalia mwezi Julai. Serikali haikutoa idadi ya vifo. Mapema mwezi wa Agosti, Ujumbe wa Kusaidia Utulivu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM) ulianzisha “mashambulizi makubwa” kuuteka tena mji wa Bariire, katika eneo la Lower Shabelle, lililoko takriban kilomita 100 magharibi mwa mji mkuu wa Somalia.
mji wa Bariire, ambao ulikuwa na kambi kubwa ya kijeshi, ilianguka bila mapigano mwezi Machi mikononi mwa Al Shabab, baada ya jeshi kuondoka, ambao waliharibu daraja muhimu, ambalo lilikuwa likitumia na jeshi kwa usmbazaji chakula. Zaidi ya wanajeshi 10,000 wa AUSSOM wapo nchini Somalia, lakini hii haiwazuii Al Shabab kuendelea kufanya mashambulizi. Licha ya hali hii ya wasiwasi, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud anashinikiza nchi hiyo kufanya uchaguzi wake wa kwanza wa moja kwa moja mwaka ujao.