
Hatimaye kocha anayatakiwa na Yanga Romuald Rakotondrabe amewaaga mabosi wake kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Madagascar na kuwaambia kuwa anakuja Tanzania kufundisha soka.
Hizi karibuni kumekuwa na taarifa mbalimbali zikisema kuwa Yanga ipo kwenye hatua ya mwisho ya kuachana na kocha wake mkuu Roman Folz kutokana na mabosi wa timu hiyo pamoja na baadhi ya mashabiki kutoridhisha na kiwango cha timu hiyo.
Yanga chini ya Folz imefanikiwa kucheza michezo mitano ya mashindano ikishinda minne na kutoka sare mmoja, ikianza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao waliibuka na ushindi wa bao 1-0, zikafuata mechi mbili dhidi ya Williete ambapo ilishinda kwa jumla ya mabao 5-0, mechi mbili ilizocheza za Ligi Kuu Bara ni dhidi ya Pamba ambapo ilishinda mabao 3-0 pamoja na mechi dhidi ya Mbeya City ambayo ilitoka suluhi.
Ujio wa Rakotondrabe maarufu kama Roro ambaye timu yake ilikuwa hapa nchini siku chache zilizopita ambapo ilishiriki michuano ya CHAN ambayo iliandaliwa na nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda umechagizwa zaidi na bosi mmoja wa idara ya ufundi kutoka Shirikisho la Soka Madagascar aliyesema kocha wao huyo ataondoka na anakuja Tanzania.
“Roro ametuambia anaondoka hapa kwetu na ametuambia anakuja huko Tanzania. Tulitaka kumbakisha lakini naona amesisitiza sana amepata ofa nzuri na klabu kubwa.
“Huyu ni kocha wa kisasa sana anafundisha soka zuri. Kwa muda aliokaa hapa kwetu ametuboreshea viwango vya wachezaji tunaamini kuwa huko atafanya mambo makubwa,” amesema bosi huyo.
Hata hivyo, taarifa za leo jioni zinafichua kuwa tayari Yanga wameshazungumza na Folz na kufikiwa makubaliano ya kuachana na muda wowote watatangaza jambo hilo la umma.
Hata hivyo pamoja na kiwango inaelezwa kuwa Yanga inalazimika kuachana na Folz kutokana na presha iliyopo nje ya uongozi kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo ambao hawakubaliani na soka la kocha huyo Mfaransa licha ya kutopoteza mechi yoyote ya mashindano msimu huu.
Rakotondrabe maarufu kwa jina la ‘Roro’ sio jina geni kwani alikuwa hapa nchini kwani wakati wa Fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) aliiongoza Madagascar kumaliza nafasi ya pili baada ya kupoteza mechi ya fainali kwa mabao 3-2 dhidi ya Morocco.
Yanga imevutiwa na ubora wa Roro na yeye akavutiwa na mradi wa klabu hiyo ambapo hatua iliyosalia ni uongozi wa Yanga kumalizana na Folz kisha jamaa atue nchini.
Awali, Yanga ilikuwa inafikiria kumrudisha Sead Ramovic ambaye yupo CR Belouizdad alikotua baada ya kutokea Jangwani, lakini dili hilo lilishindwa kukamilika.
Mwananchi linafahamu kwamba Roro ameshaanza kufuatilia mafaili mbalimbali ya mechi za timu hiyo kisha kuwaambia mabosi wa Yanga wapi timu yao inakwama.
Roro (60), aliingia kwenye rada za Simba wakati ikitafuta mrithi wa Fadlu Davids, lakini mambo mawili yakaua dili hilo ikiwemo mshahara alioutaka na namna anavyotaka benchi lake liwe katika kikosi hicho.
Kocha huyo anamiliki leseni ya Uefa Pro ambayo inakidhi vigezo vya kuiongoza timu yoyote Afrika katika mashindano mbalimbali.