India. Shah Rukh Khan na Kajol ni kati ya majina makubwa katika kiwanda cha filamu India, Bollywood.
Wawili hao wanatajwa ni waigizaji walioteka hisia za wengi siyo India pekee, bali duniani kwa ujumla kutokana na kucheza filamu nyingi za mapenzi.
Nyimbo nyingi na filamu za Kihindi zinafuatiliwa sana kwa sababu yao na wakipewa nafasi pamoja wanaitendea haki, iwe ni ngoma au filamu na kolabo yao imesababisha wengi waamini walishatoka kimapenzi nje ya kazi hiyo.
Kwa hivyo mashabiki wamejikuta wakiwa na maswali kichwani juu ya uhusiano wao, huku Khan akiwa kwenye ndoa na mkewe Gauri Rukh Khan tangu mwaka 1991 na wana watoto watatu, huku Kajol ni mke wa Ajay Devgn tangu mwaka 1999 na wana watoto wawili.
Wote wawili wamekuwa waaminifu kwenye ndoa zao na wamekuwa wakikanusha uvumi wa kuwa katika uhusiano ambao wengi wanatamani ungekuwa kweli au kama vipi wawe tu wapenzi kutokana na kuvutiwa na kombo hiyo.
Mashabiki wengi hawaamini kama wawili hawa sio wapenzi kutokana na wanavyokuwa karibu ikiwamo kwenye uzinduzi wa filamu na wamekuwa wakiandika mitandaoni wanavyotamani wawe wapenzi kwani wanaendana.
Hapa ni kazi zao ambazo zimechangia kuwachanganya mashabiki wasiojua historia yao na zimewaaminisha ni wapenzi kweli na hata walipojua ukweli hawakuamini na kutamani ingekuwa hivyo.

1. Baazigar (1993)
Ni filamu ya mwaka 1993 iliyoongozwa na Abbas Mustan iliyobeba msisimko mkubwa. Katika filamu hii, Khan amecheza kama mhusika mpole na Kajol ni mwenye tabia njema.
Pia ina misukosuko na ulipaji wa kisasi vilivyoifanya kuvutia na kufuatiliwa sana.
Wawili hao pia walitokea kwenye wimbo ulioibeba filamu hiyo, wakiigiza sauti za wanamuziki wakongwe India, Kumar Sanu na Alka Yagnik na wimbo huo ni kati ya zinazofanya vizuri hadi sasa.

2 Dilwale Dulhania Le Jayenge (DDLJ, 1995)
Filamu hiyo iliyoongozwa na muongozaji maarufu Aditya Chopra (1995), inatajwa ni moja ya filamu za mapenzi bora katika historia ya Bollywood.
Hadithi inamhusu Raj (Shah Rukh Khan) na Simran (Kajol), wanaopendana tangu walipokutana kwenye safari ya Ulaya, lakini wakakumbana na changamoto zinazotokana na mila, familia na tofauti za tamaduni.
Katika filamu hiyo, wawili hao walionyesha kuelewana na kama kawaida ya India ikatoka na nyimbo ambayo pia walihusika wakiigizia sauti ya wanamuziki wakongwe Lata Mangeshkar na mwanamama Udit Narayan.

3 Kabhi Khushi Kabhie Gham (2001)
Filamu ya kifamilia yenye hisia nyingi ya mwaka 2001, iliyotungwa na Karan Johar. Ni hadithi ya upendo, kutenganishwa na familia na kisha wanakutana tena.
Katika filamu hiyo Khan aliigiza kama Rahul, mwana wa familia tajiri na Kajol anaigiza kama Anjali, mke wake. Filamu inaangazia jinsi upendo unavyoweza kuzungukwa na tofauti, misukosuko ya kijamii na maamuzi magumu ya familia.
Uhusiano wao umetiliwa mkazo hasa kutokana na migongano ya kifamilia, mshikamano na hisia wakati wanapitia vipindi vigumu hasa vya kukataliwa na familia.
Baada ya filamu hiyo kufanya vizuri kampuni ya usambazaji wa muziki India ikachangamkia fursa ya kutengeneza wimbo ulioimbwa na mwanamama mwenye sauti ya kipekee Lata Mangeshkar.
Lakini kwenye video ya wimbo huo alikuwepo Shah Rukh pekee akisaidiana na Rani Mukerji ambaye ameigiza naye kwenye filamu mbalimbali kama Chalte Chalte (2003),
Kabhi Alvida Naa Kehna (2006), Paheli na nyinginezo.

4. Kuch Kuch Hota Hai (1998)
Filamu hii ilitoka mwaka 1998. Ni moja ya filamu maarufu za Bollywood iliyompa Khan na Kajol umaarufu mkubwa wa mapenzi kwenye skrini.
Khan kama Rahul na Kajol kama Anjali, inaeleza hadithi ya marafiki wanaoweza kuwa wapenzi na Rahul hajui kama Anjali ana hisia kwake na yeye mwenyewe amependezwa na msichana mwingine (Tina).
Hadithi hii imebeba mambo mengi ikiwamo mabadiliko ya kimahusiano, uvumilivu na kujitolea, ikionyesha zaidi kutoka uhusiano wa rafiki hadi wapenzi.
Filamu hiyo iliwafanya wasanii hao hasa Khan kupendwa na wanawake kutokana na pendo aliouonyesha kuanzia kwenye filamu hadi kwenye video ya wimbo wenyewe.
Aliuvaa uhusika haswa kwenye wimbo huo ulioimbwa na mkongwe Udit Narayan, Alka Yagnik na Kumar Sanu kiasi cha baadhi ya mashabiki hadi leo kuamini wimbo wa Kuch Kuch uliimbwa na SRK na Kajol lakini ukweli ni wao waliigiza tu.

5. My Name Is Khan (2010)
Khan na Kajol walikutana tena katika My Name Is Khan mwaka 2010. Khan alicheza kama Rizwan Khan mwanamume muislamu mwenye hali ya Asperger’s Syndrome (mtu mwenye changamoto ya kuelewa hisia au lugha ya mwili ya wengine) ambaye anachukua doria ya kuhakiki jina lake kwa Rais wa Marekani baada ya kukabidhiwa lawama zisizo haki kutokana na dini.
Kajol anacheza kama Mandira, mke wake ambaye anakabili huzuni ya kupoteza mtoto wao kutokana na uonevu wa chuki ya kijamii. Filamu hii inachanganya hadithi ya upendo na shida za jamii, ikionyesha mapenzi hayana rangi, dini wala mipaka ya kijamii.
Uhusiano wao unaangazia mambo mbalimbali si mapenzi pekee, bali pia kuwa na imani, ugumu na uvumilivu.
Filamu hiyo ilikuwa kama mwendelezo wa kile walichokifanya kwenye filamu zingine na machoni mwa mashabiki waliamini wawili hao ni mke na mume.

6. Dilwale (2015)
Dilwale (2015) iliwakutanisha tena wawili hao baada ya kukaa miaka mitano bila ya kuonekana pamoja. Katika filamu hiyo khan alicheza kama mhusika aliyebadili tabia na Kajol ni mpenzi wake. Walipendana lakini familia zao ni wa makundi ya uhalifu yanayopingana. Kama ilivyo filamu nyingine kolabo yao ilibamba kwa hisia kali na mashabiki walifurahia kuona wawili hao wakirudi pamoja.