Riyadh, Saudi Arabia. Cristiano Ronaldo ametangazwa kuwa bilionea wa kwanza mwanasoka baada ya kukamilika kwa hesabu za utajiri wake wa kushangaza.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40 anasemekana kuwa na utajiri wenye thamani ya Pauni 1.04 bilioni (Sh3.4 trilioni) baada ya wataalamu wa masuala ya ukaguzi wa fedha wa taasisi ya Bloomberg kuzama kwa kina katika mapato yake ya kazi, uwekezaji na mikataba ya matangazo ambavyo vyote vimerekebishwa kwa viwango vya kodi vilivyokuwepo na utendaji wa soko.

Wanaripoti kwamba ubashiri wa fedha za Ronaldo nchini Saudi Arabia ‘umempandisha kileleni mwa chati ya wanamichezo wanaolipwa pesa nyingi zaidi’.

Ndiye mwanasoka wa kwanza katika Orodha yao mpya ya Mabilionea ya Bloomberg na wanabainisha kuwa utajiri wake sasa unamuacha kwa mbali mpinzani wake wa muda mrefu Lionel Messi baada ya Muargentina huyo kuamua kuhamia Marekani na Inter Miami.

Ronaldo ana mkataba wa maisha na Nike ambao unaripotiwa kuwa na thamani ya Pauni 745 milioni (Sh2.5 trilioni) kwa jumla ambao una thamani kubwa zaidi kuliko kampuni yoyote.

Ni mshirika pia wa kampuni za Tag Heur, Armani, PokerStars, Samsung, Unilever, Louis Vuitton na nyinginezo.

Kwa sasa anajenga jumba la kifahari linalogharimu Pauni 28 milioni (Sh92 bilioni), ambapo matoleo ya kifahari yamepambwa kwa vito na saa za bei ghali zaidi duniani, ikiwa ni pamoja na Franck Muller Invisible Baguette Diamonds Imperial Tourbillon vyenye thamani ya Pauni 1.13 milioni (3.7 bilioni).

Ronaldo analipwa Pauni 300 (Sh989,857) kwa dakika nchini Saudi Arabia lakini Jumanne usiku alikiri kwamba anatamani angeondoka na kuichezea timu ya taifa ya Ureno pekee.

Al-Nassr wanatumia Pauni 167.9 milioni (Sh554 bilioni) kumlipa kwa mwaka kwenye kandarasi ya Ronaldo hivyo hapana shaka kauli hiyo hawajaipokea vizuri.

Ronaldo pia ana hisa katika klabu hiyo jambo linalomuomgezea thamani zaidi. Lakini pamoja na hilo, Ronaldo anaonekana anaiwaza zaidi timu ya Taifa ya Ureno na hilo amelithibtisha wakati akitwaa tuzo ya Globo Prestigio kwa mchango wake bora katika soka kwa nchi yake.

Akiwa jukwaani katika Ukumbi wa FPF Arena Ureno mjini Oeiras, Ronaldo alisema daima anatamani kuitumikia Ureno.”

Nimekuwa na timu ya taifa kwa miaka 22. Nadhani hilo linajieleza lenyewe. Shauku niliyo nayo ya kuvaa jezi, kushinda mataji na kuchezea timu ya taifa.

“Mara nyingi nasema kama ningeweza, ningecheza soka kwa ajili ya timu ya taifa pekee. Nisingechezea klabu nyingine yoyote kwa sababu ni kilele na kilele cha mchezaji wa soka,” alisema Ronaldo.

Ronaldo anaonekana yuko katika hali nzuri ya kimwili na bado anacheza kwa kiwango cha juu akiwa na umri wa miaka 40.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *