Beki wa zamani wa kushoto wa Barcelona na timu ya Taifa ya Hispania, Jordi Alba ametangaza rasmi kustaafu soka la kulipwa akiwa na umri wa miaka 36.
Alba ametangaza kustaafu ikiwa ni siku chache tangu rafiki yake na nyota mwenzake wa zamani wa Barcelona na Hispania, Sergio Busquets kuchukua uamuzi kama huo.

Beki huyo wa kushoto, kama ilivyo kwa Busquets naye amestaafu huku akiwa anaitumikia Inter Miami FC inayoshiriki Ligi Kuu Marekani (MLS).
Mkataba wa Alba na Inter Miami ilikuwa ufikie tamati mwaka 2027 lakini sasa ameamua kuukatisha kwa lengo la kupumzika moja kwa moja.

Alba anastaafu akiwa ameshinda idadi ya mataji 22 tofauti kwa ngazi ya klabu na timu ya taifa huku mengi yakiwa ni yale aliyonyanyua akiwa na Barcelona.
Akiwa na Barcelona, Alba ametwaa mataji 17 ambapo sita ni ya Ligi Kuu ya Hispania, moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, matano ya Supercopa de Espana, moja la Klabu Bingwa ya Dunia na matano ya Copa del Rey.

Nyota huyo amesema kuwa anaondoka huku akiwa na heshima kubwa na mchezo wa soka kwa vile umekuwa na maana kubwa kwake.
“Asanteni sana mashabiki wote kwa ukarimu wenu. Mmenifundisha kwamba jezi haivaliwi tu bali inatakiwa iwe kwenye hisia.
“Leo ninafunga ukurasa wangu nikifahamu nimetoa kila kitu. Mpira wa miguu umekuwa na siku zote utakuwa sehemu muhimu katika maisha yangu. Asante soka kwa kila kitu,” amesema Alba.