London, England. Kigogo Brooklyn Earick ameamua kuondoa rasmi ofa yake ya Pauni 4.5 bilioni ya kuinunua klabu ya Tottenham Hotspur, baada ya familia ya Lewis kusisitiza hawatoiuza kwa pesa yoyote ile.

Gazeti la The Sun limefichua Earick, aliyewahi kuwa DJ mwenye umri wa miaka 41, alikuwa ameungana na kikundi cha wawekezaji 12 kutoka Marekani ili kuinunua Spurs kwa dau la rekodi ya dunia.

Earick alikuwa ameandaa mpango wa kuinunua timu hiyo kwa Pauni 3.3 bilioni, pamoja na nyongeza ya Pauni 1.2 bilioni ambazo zingetumika kama ada za usajili, mishahara na ada za mawakala.

Licha ya wamiliki wa sasa wa Spurs, kampuni ya ENIC na familia ya Lewis kukataa ofa hiyo waziwazi, taarifa kutoka Soko la Hisa la London, zimefichua mazungumzo ya kina kati ya pande zote mbili yalifanyika wiki iliyopita.

Hata hivyo, baada ya familia ya Lewis kueleza wazi haina mpango wowote wa kuuza klabu na badala yake inataka kuendelea kuiendeleza, Earick alikubaliana na kuondoa rasmi pendekezo lake la kuinunua.

Kwa mujibu wa tovuti ya The Sun, Earick alifanya mazungumzo ya moja kwa moja na Douglas Armstrong, mshauri wa kisheria wa familia ya Lewis kuhusiana na mpango huo wa kuinunua Spurs licha ya kufuata taratibu nyingine.

Baada ya kuondoa ofa yake, Earick alitoa ujumbe wa heshima katika akaunti yake ya X (Twitter) akisema:

“Imekuwa heshima kubwa kuzungumza na wawakilishi wa Tottenham Hotspur na familia ya Lewis katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Ninaiheshimu sana klabu, uongozi wake na mashabiki wake na nawatakia kia heri.”

Licha ya pande zote kuhitimisha rasmi mazungumzo, makubaliano hayo hayajazuia uwezekano wa kuwasilishwa ofa nyingine siku za usoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *