
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, juma hili walieleza wasiwasi wao kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Burundi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa wataalamu hao, vitendo hivi vinatekelezwa na maofisa wa usalama wa Serikali au na watu binafsi wanaofanya kazi kwa kushirikiana na mamlaka, huku wahusika wakishindwa kuchukuliwa hatua.
Wataalamu hao wamesema kati ya Januari 2024 na Mei 2025, mashirika ya kiraia ya Burundi yalirekodi angalau matukio 200 ya unyanyasaji wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa watoto.
Aidha mashirika hayo yalirekodi matukio 58 ya watu kupotezwa, 62 ya utesaji, 892 ya kuzuiliwa kinyume cha sheria na 605 ya mauaji ya kupangwa.
Kwenye taarifa yao, wataalamu hao wa umoja wa mataifa wameoneshwa kuguswa na ukweli kuwa ukiukwaji huu mkubwa wa haki za binadamu unatumiwa kuwatisha wananchi wakati wa kipindi cha uchaguzi, kwa manufaa ya chama tawala.
Katika uchaguzi wa mwezi Juni mwaka huu, chama madarakani CNDD-FDD kilipata asilimia 96 ya kura zote na viti vyote 100 bungeni.
Rais Evariste Ndayishimiye ambaye aliingia madarakani 2020 baada ya kifo cha mtangulizi wake, Pierre Nkurunziza, aliyetawala kwa mkono wa chuma kwa miaka 15, aliahidi kuleta mabadiliko ya mfumo wa utoaji haki, hata hivyo miaka mitano baadae utawala wake unatuhumiwa kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.