
Oktoba 14 kila mwaka ni Nyerere Day ambayo hutumika kuadhimisha kifo cha mwasisi wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere ‘Baba wa Taifa’, na binafsi natamani tumtumie Nyerere kama kioo kujitazama tulipotoka, tulipo na tunapokwenda.
Siku zote kioo kina sifa moja kuu, hakidanganyi, kwa hiyo kama sote tunakubali Nyerere ni baba wa Taifa, basi tumtumie kama kioo kujitazama sura yetu kama Taifa inafananaje katika nyakati hizi ikiwa ni miaka 26 baada ya kifo chake kilichotokea Oktoba 14, 1999.
Licha ya kwamba hatuko naye kimwili, lakini kauli zake na falsafa zake zinaishi hadi leo hii kiasi kwamba, ukisikiliza hotuba yake ya mwaka 1965 leo akikemea au kuonya kuhusu jambo fulani, utadhani ndio ameongea leo kwa nyakati tulizonazo.
Mwaka 1995, Nyerere alikemea kwa nguvu zote chembechembe za udini na ukabila, lakini katika siku za karibuni pepo hili linaonekana kurejea kwa kasi nchini, jambo ambalo halina afya na limeanza kutugawa kama Taifa, tunapaswa kujitafakari.
Nikimnukuu Nyerere, alisema “Mambo ya kuchochea chuki za ukabila ama dini yakianza na tukayapa nafasi, hayana simile.” Baba wa Taifa akaenda mbali na kutolea mfano wa Rwanda ambapo Watutsi na Wahutu walivyochinjana 1994.
Lakini leo Watanzania wanathubutu kumsema Rais wetu Samia Suluhu Hassan na kumtambulisha kama ‘mzanzibar’ badala ya kumtambulisha kama ‘Mtanzania’ na huko mitandaoni wanajadili watu kwa dini zao badala ya utanzania wao.
Rais Samia yuko madarakani kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, hayuko pale kwa sababu ni Mzanzibar au Mwislamu. Ni muhimu sana ukaelewa hili na tuchukue tahadhari kubwa na huu mwelekeo tunaotaka kuuchukua.
Ndio maana nimetangulia kusema hebu tumfanye Nyerere ndio kioo chetu, halafu tujitazame kama tuko na sura ile ile (Taifa) aliloliasisi na kutuachia 1999, na kama silo alilotuachia basi tutafute wapi tulipojikwaa na sio tulipoangukia.
Nyerere ni kiongozi aliyehubiri haki akitambua kuwa haki ndio ambayo huzaa amani na hili alilitilia mkazo Julai 27 mwaka 1970 katika hotuba ya ufunguzi wa Semina ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini iliyofanyika mjini Tabora.
Nyerere alisema kelele za dhuluma zinapoanza kutoka kwa maskini kuwa wanadhulumiwa na matajiri “misikiti kimya, makanisa kimya; hayasemi kitu. Yanasema: “Wana fujo hao” na hasa kama wanaodhulumu ni Serikali”
Baba wa Taifa akasema pale inapotokea Serikali ndio inayodhulumu basi “mapadri (baadhi) mara wanasimama katika Makanisa wanasema:- “Mpeni Kaisari kilicho chake”, mwisho wa kunukuu hotuba hiyo ya mwasisi wa Taifa la Tanzania.
Hata leo hii ninapoandika makala hii, ingawa sio viongozi wote wa dini hukaa kimya haki inapokandamizwa, lakini baadhi kama si wengi, wanachukulia msemo wa ‘mpe kaisari kilicho chake’, kama kisingizio cha kukwepa wajibu wao.
Martin Luther King ambaye aliheshimika duniani na si kwa Wakristo pekee aliwahi kusema “Injustice anywhere is a threat to justice everywhere”, kwa Kiswahili alimaanisha “Udhalimu popote pale ni tishio kwa haki kila mahali”.
Lakini Dk Nazir Khan alipata kusema “As custodian of God on earth, establishing justice for all people is for utmost importance, and hence it is those who stand for justice who receives divine aid regardless of their ideological affiliation”.
Kwa tafsiri isiyo rasmi alimaanisha: “Kama mlinzi wa Mungu duniani, kusimamia uadilifu kwa watu wote ni jambo la maana sana, na kwa hiyo ni wale wanaosimamia haki ndio wanaopokea msaada wa kiungu bila kujali itikadi zao za kidini.”
Sasa tunapoadhimisha Nyerere Day, tusiishie tu kusifia kazi zake, misimamo yake na falsafa zake, hapana, viongozi wa dini wasimame kuhesabiwa tujue ni wa ngapi wanaosimama upande wa haki, ili tuwajue wanaomuenzi Nyerere kivitendo.
Nyerere alipotoa kauli hiyo, japo aliwalenga viongozi wa dini kwa kuwa alikuwa anazungumza katika jukwaa la viongozi wa dini, alipeleka ujumbe wa haki kwa kila mtu, kuanzia viongozi wa dini, wanasiasa, watawala na sisi raia wa kawaida.
Baba wa Taifa aliondoka akiwa ametuachia Taifa lenye watu wenye hofu ya Mungu, wenye utu, wanaothamini haki ya kuishi, wenye upendo na mshikamano, lakini leo tukiweka kioo mbele na kujitazama, bado tutakuwa na sura hiyo?.
Tunapozungumzia haki, tuihubiri haki hii katika chaguzi zetu, tuhubiri haki katika mahakama zetu, tuhubiri haki katika huduma za kijamii na tusiishie kuhubiri tu amani… amani… amani bila kufahamu kuwa bila haki hiyo amani haiwezi kuwepo.
Kuna nukuu maarufu sana ya baba wa Taifa inayohamasisha vijana kupinga mifumo dhalimu na akataka Taifa lenye vijana wenye kujiamini na sio waoga.
“Tunataka kuona vijana wenye ujasiri wa kuhoji na kupiga vita mifumo ya kidhalimu isiyoshabihiana na matakwa na matarajio ya jamii ya Kitanzania. Tunataka vijana waasisi mifumo kandamizi, ubwana na ufisadi katika Taifa,”alisema.
Lakini tunapomuenzi leo, kwa hizi doria mtandaoni, vijana wakosoaji wako salama au ndio sehemu ya hao tunaowasikia wamepotea au kutekwa? Ama tumegeuza ukosoaji kama ni dhambi lakini ‘uchawa’ ndio uzalendo.
Mimi natamani namna hii, kwa kuwa Tanzania inaheshimu na kufuata utawala wa sheria, basi wale wanaovuka mipaka katika ukosoaji wao na kuvunja sheria wapelekwe mahakamani na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.
Mwaka 1962, Nyerere aliandika kitabu kinaitwa “Tujisahihishe”, humo aliorodhesha makosa aliyosema yanatokana na ubinafsi na akawaasa Watanzania wajiepusha nayo, najiuliza tukiweka kioo leo tutakuwa tumemuenzi katika hilo?
Nyerere aliandika na nanukuu, “Kosa lingine linalotokana na ubinafsi tunalifanya wakati wa kuchagua viongozi. Wakati mwingine hufanywa na wanachama (wa vyama vya siasa) na wakati mwingine hufanywa na viongozi wenyewe.”
Akaongeza kusema: “Viongozi wetu hawana budi watokane na watu, bila hila, vitisho, rushwa au ujanja wa aina yoyote,”mwisho wa kunukuu.
Sasa tuweke kioo hiki cha Nyerere na tujitazame namna tunavyopata viongozi wetu, kuanzia wa kiti cha Rais, ubunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa ni kweli tunawapata kwa haki na usawa bila figisu figisu zozote?.
Ukiondoa mapungufu ya aina hiyo ambayo ni ya kila binadamu, lakini Nyerere alikuwa na ujasiri wa kukiri makosa aliyoyafanya na si viongozi wengi duniani walio na ujasiri wa aina hiyo, ni viongozi wetu wangapi wa sasa wana ujasiri huo?.
Kwa hiyo, tunapoadhimisha Nyerere Day, ni muhimu sana tukamtumia Nyerere kama kioo kujitazama kama Taifa, na tujikiri kwa nafsi yetu kama kweli hili ndilo Taifa alilotuachia, kama sio, basi tutafakari wapi tulipojikwaa tuchukue hatua.
Tumtumie Nyerere kama kioo kujitazama tulipotoka, tulipo na tunapokwenda wala tusione haya kujisahihisha, kwa sababu hiyo ndio njia pekee ya kuliponya taifa na wala hatujachelewa.
Ninamshukuru na kumpongeza mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya CCM, Rais Samia pamoja na CCM yenyewe, wameahidi kuleta maridhiano ya kitaifa endapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi, huu uwe mwelekeo kwetu sote.
0656600900