Mbeya. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, ameongoza wananchi na viongozi mbalimbali katika ibada maalumu ya kumuombea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akiwaomba kufuata mema yote aliyoyafanya.

Ibada hiyo iliyofanyika leo, Oktoba 14, 2025, katika Kanisa Katoliki Mwanjelwa, ikiwa ni kumbukizi ya miaka 26 ya kifo chake, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Akizungumza katika ibada hiyo, Dk Mpango amewaomba wananchi na viongozi kufuata mema aliyofanya Mwalimu Nyerere na kumuombea ili awe sehemu ya watakatifu.

Pia, amemuomba na kumuelekeza Waziri Mkuu Majaliwa kutumia mamlaka yake kuhakikisha maombi yaliyosomwa na viongozi wa dini yanatumika kwenye vyombo vya habari, hasa Radio Tanzania.

“Niwashukuru na kuwapongeza kwa ibada njema, hasa viongozi tufuate yale aliyofanya hayati Nyerere. Kila mmoja kwa nafasi yake amuombee ili awe sehemu ya watakatifu huko alipo,” amesema Dk Mpango.

Awali, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Gervas Nyaisonga, amesema Nyerere alikuwa mtu mwenye mwenendo wa huruma, upendo na uaminifu, hali hiyo hufanya mtu kuwa mtakatifu bila kujali itikadi zake za kidini.

Amesema mchakato wa kufikia utakatifu ni kupewa hadhi ya utumishi kwa kuzingatia hisia hasa katika jimbo lake la utumishi, mwenye fadhila kuu, kisha kutangazwa mtu kuwa mwenye heri.

“Hatua ya mwisho ni kuwa mtakatifu ambaye amehakikishiwa na Kanisa kwamba yuko mbinguni, hivyo, mchakato wa Nyerere kutangazwa upo hatua ya kwanza na hatua hii itachukua muda mrefu.

“Mchakato unaendelea na tutatangaza akifikia hatua ya kuwa mtakatifu. Anahisiwa kuwa hivyo kutokana na alivyothibitisha, alikuwa mfuata maadili, haki, mnyenyekevu na mwaminifu,” amesema na kuongeza:

“Anaweza kutajwa kuwa miongoni mwa watakatifu, akiwamo Papa aliyefariki mwaka 202, Mwalimu Nyerere alijitahidi kutokuwa mnafiki wa Mafarisayo. Urithi aliotuachia ulidhihirisha utakatifu katika siasa, demokrasia, maisha ya kijamii na kiuchumi,” amesema Nyaisonga.

Nyaisonga ameongeza kuwa Mwalimu Nyerere aliacha pia urithi wa elimu na kufanya lugha ya Kiswahili kutumika kimataifa, na alionesha uadilifu katika utumishi bila kuweka maslahi binafsi.

Amesema hata baada ya kustaafu alikuwa akitoa maoni yake bila kusita kwa mustakabali wa nchi, na kwamba Kanisa Katoliki linahisi hayati huyo amepewa utakatifu na Mungu.

“Kama tunatamani kuwa watakatifu, tutumie Mwalimu Nyerere kuwa kielelezo. Tujiulize tumefanya au tutafanya nini ili kuwa watakatifu. Tunapotendeana ubaya baina ya binadamu au Watanzania, tukumbuke kuwa kiama kipo na tutaulizwa,” amesema.

Amesema bado muda upo wa kila mmoja kujitafakari, kwani Mungu ni mwenye huruma na mwenye kusamehe, na kuwaomba Watanzania kumuombea Mwalimu Nyerere.

Akitoa salamu za Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Mkoa huo, Beno Malisa, amewashukuru viongozi wa dini na wananchi kwa ibada hiyo, akiomba washiriki pia katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge.

“Niwashukuru viongozi wa dini na wananchi wote kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi katika ibada hii. Niwaombe pia kushiriki kilele cha mbio za Mwenge hapa Mbeya,” amesema Malisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *