Manchester, England. Marcus Rashford ametaja mazingira yasiyo rafiki ya Manchester United kuwa moja ya sababu zilizomfanya kushindwa kudumisha kiwango cha juu mara kwa mara katika maisha yake ya soka huko Old Trafford.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 27 aliondoka Old Trafford msimu uliopita kwa mkopo wa mwaka mmoja kwenda Barcelona, ambapo anaweza kujiunga na Klabu hiyo kutokana na kiwango anachokionyesha hadi sasa.

Rashford amekuwa na mwanzo mzuri nchini Hispania, akifunga mabao matatu na kutoa pasi tano za mabao katika mechi 10. Hali hiyo imemuwezesha kubaki kwenye kikosi cha England kinachoongozwa na Thomas Tuchel tayari kwa maandalizi ya Kombe la Dunia 2026.
Akizungumza na ITV kabla ya mchezo wa England dhidi ya Latvia, Rashford alikubali kwamba anahitaji kuwa mchezaji wa kiwango cha juu kila mara, lakini alionyesha kwamba hali aliyoikuta United ilimzuia kufikia kiwango hicho.

“Ni kweli, kudumu kwenye kiwango bora ni muhimu sana, Nimekuwa katika mazingira yasiyo thabiti kwa muda mrefu, na kufanya kuwa thabiti ni ngumu zaidi. Lakini sasa nataka kuboresha hili na kuonyesha kiwango changu mara kwa mara. Ninapokuwa bora, nacheza kwa furaha kubwa, amesema Rashford.
Rashford alianzia maisha yake ya soka chini ya kocha, Louis van Gaal mwaka 2016 na kucheza na makocha wengi wa kudumu na wa muda mfupi. Aliweza kufikia kiwango bora zaidi akiwa na Ole Gunnar Solskjaer, ambapo alifunga mabao 22 na kutoa pasi 9 msimu wa 2019-20, kisha akafunga 21 na kutoa pasi 13 msimu uliofuata.

Hata hivyo, kiwango chake kilipungua sana baada ya Solskjaer kuondolewa, na kupelekea kipindi kigumu chini ya makocha waliofuatia.
Alikua bora tena chini ya Erik ten Hag msimu wa 2022-23 akiwa amefunga mabao 30 katika mashindano yote, lakini alikumbwa na kushuka kwa kiwango msimu uliofuata, jambo lililozua tahadhari kutoka kwa kocha ten Hag kuhusu mtindo wake wa maisha.

Rashford alipelekwa kwa mkopo Aston Villa msimu uliopita, akifunga mabao 4 na kutoa pasi 6, na sasa anaendeleza vizuri akiwa na Barcelona. Wakurugenzi wa Barcelona wamesema wanaridhika na Rashford na wako wazi kumfanya mchezaji wa kudumu.
Deco, mkurugenzi wa michezo wa Barcelona, amesema: “Yeye ni mchezaji wa kiwango cha juu. Alipata mafanikio makubwa mapema, lakini kipindi cha mabadiliko makubwa ya makocha United kilimchanganya. Tunafurahi naye, na hiyo ndiyo muhimu zaidi.”