
Ripoti iliyotolewa mjini Geneva Uswisi inasema kuongezeka huko kumesababishwa na uzalishaji unaoendelea wa kibinadamu, ongezeko la matukio ya moto wa nyika, na kupungua kwa uwezo wa ardhi na bahari kufyonza hewa chafuzi hali ambayo inatishia kuunda mzunguko hatari wa mabadiliko ya tabianchi.
Ongezeko mara tatu tangu miaka ya 1960
Ripoti hiyo mpya ya WMO kuhusu gesi chafuzi inaonesha kwamba kasi ya ongezeko la hewa ukaa imeongezeka mara tatu tangu miaka ya 1960, kutoka wastani wa ongezeko la kila mwaka la sehemu 0.8 kwa milioni (ppm) hadi 2.4 ppm kwa mwaka katika muongo wa 2011 hadi 2020.
Kiwango hicho kiliruka kwa ongezeko la kuvunja rekodi la 3.5 ppm kati ya mwaka 2023 na 2024 ambbalo ni ongezeko kubwa zaidi tangu ufuatiliaji ulipoanza mwaka 1957 imesema WMO.
Ripoti imetanabaisha kwamba kiwango cha wastani cha hewa ukaa kilifikia 423.9 ppm mwaka 2024, kikitoka 377.1 ppm wakati taarifa hiyo ilipochapishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2004.
Takribani nusu ya hewa ukaa inayotolewa hubaki angani, imesema ripoti huku sehemu iliyobaki ikifyonzwa na ardhi na bahari, ambapo sasa uwezo wa kufyonza unazidi kudhoofika kutokana na kupanda kwa joto, ambalo hupunguza uwezo wa bahari kufyonza gesi chafu na kuongeza ukame.
Kuongezeka kwa hewa ukaa mwaka 2024 kunadhaniwa kuchochewa zaidi na ongezeko la matukio ya moto wa nyika na kupungua kwa ufyonzaji wa hewa ukaa wa ardhi na bahari katika mwaka huo ambao ulikuwa mwaka wenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa, ukiwa na athari kubwa ya hali ya hewa ya El Niño.
Oksana Tarasova, afisa mwandamizi wa kisayansi wa WMO aliyeratibu utafiti wa ripoti hiyo amesema “Kuna wasiwasi kuwa uwezo wa ardhi na bahari kufyonza hewa ukaa unazidi kupungua, jambo ambalo litaongeza kiasi cha hewa ukaa kinachobaki angani, na hivyo kuharakisha ongezeko la joto duniani. Ufuatiliaji endelevu na wenye nguvu wa gesi chafuzi ni muhimu ili kuelewa mizunguko hii.”
Rekodi nyingine za juu
Gesi nyingine mbili muhimu chafuzi zenye kudumu kwa muda mrefu kwa mujibu wa ripoti ni ya methane (CH₄) na nitrous oxide (N₂O) ambazo pia zimeelezwa zimefikia viwango vipya vya juu vya utoaji hewa hiyo.
Ripoti imeanisha kuwa kiwango cha methane kilipanda hadi sehemu 1,942 kwa bilioni (ppb), sawa na ongezeko la asilimia 166 juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda, huku nitrous oxide ikifikia 338 ppb, ambalo ni ongezeko la asilimia 25.
Ko Barrett, ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa WMO amesema “Joto linalonaswa na hewa ukaa na gesi nyingine chafuzi linachochea zaidi hali ya hewa yetu, na kusababisha matukio zaidi ya hali mbaya ya hewa. Kupunguza utoaji wa gesi chafuzi ni muhimu si tu kwa tabianchi yetu, bali pia kwa usalama wa kiuchumi na ustawi wa jamii”.
Ufuatiliaji na hatua
WMO imetoa ripoti hii kabla ya mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi wa COP30 utakaofanyika Belém, Brazil, kuanzia mwezi Novemba, ikisisitiza kuwa ufuatiliaji wa kimataifa wa kudumu ni muhimu kwa kuongoza hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.