Video ya IOM inamuonesha mvuvi Samson Atia akiwa ziwa Victoria akimkata Samaki aliyemvua. Toka enzi na enzi familia yake imekuwa ikitegemea ziwa hili kwa ajili ya kipato na kujikimu kimaisha kama anavyoeleza.
“Baba yangu alikuwa mvuvi na hata nami sasa ni mvuvi, alinifundisha kazi za uvuvi ningali mdogo na mpaka wa leo bado naendelea na hiyo kazi ya uvuvi. Hili ziwa limenisaidia sana katika maisha yangu yote, chakula kinatoka kwa ziwa hili na vile vile watoto wanakula vizuri na wanaenda shuleni kupitia riziki ninayopata kutokana na uvuvi. Tegemeo langu ni hili ziwa.”
Faida hizo za ziwa Viktoria zinatiwa dosari na uhalifu wa kimataifa, na kuweka maisha ya jamii zinazozunguka ziwa hili hatarini kama anavyoeleza Tom Midiwo, Afisa wa Kikosi cha ulinzi wa pwani cha nchini Kenya.
“Victoria ni ziwa linaloshirikiwa na nchi tatu Kenya, Uganda na Tanzania. Tunapojua kwamba mipaka ni wazi na si rahisi kudhibitiwa, kuna mambo mengi ya haramu yanayofanyika, kama vile usafirishaji haramu wa watu. Kuna pia biashara haramu ya bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru, zikivuka mipaka ya nchi hizi. Pia tunakabiliwa na tatizo la dawa za kulevya zinazovuka mipaka kinyume cha sheria.”

Samson Atia, mvuvi katika Ziwa Victoria akiwa na wenzake waliopewa mafunzo na IOM kuhusu ujuzi wa uvuvi salama na kuzuia uhalifu.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM kwakushirikiana na wadau wanatoa mafunzo ya ulinzi wa ziwa hilo kwa pamoja kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo doria za ziwani kama anavyoeleza Paul Ochieng’ Obama, Afisa wa huduma ya uvuvi Kenya “Ofisi ya ulinzi wa maziwa CMX iliwaweka maafisa wengi katika hali halisi ya maisha, hasa katika kukabiliana na uhalifu, hususan katika usafirishaji haramu wa binadamu, uvuvi haramu usioripotiwa na usiodhibitiwa katika Ziwa Viktoria na pia, bila kusahau dawa za kulevya na usafirishaji wake.”
Mbinu nyingine ni kuelimisha kutumia michezo ambapo maafisa wa usalama na jamii, wanajenga uaminifu kupitia michezo na kuhamasisha kushirikishana taarifa kuhusu uhalifu.
Iom inasema Kwa upande wa Kenya pekee zaidi ya watu milioni 4 wanalitegemea ziwa hilo kujipatia riziki ndio maana Samson Atia anasema watu wanapaswa kuwa whistle blowers akimaanisha wawafichua wale watenda maovu.
“Tunafaa kuwa whistle blowers tukiona kitu kibaya tufikishe ripoti hiyo kwa mamlaka yanayohusika na Nyanja hiyo ili waweze kuchukua hatua haraka iwezekanavyo. Unajua shida ni huwa wananchi wanaogopa walinda amani, wanawaogopa sana, hawaoni maadui zao kama ni tishio kubwa. Tukiwa marafiki na umoja tutawezakufanya kazi Pamoja, hakuna kitu kitatuzuia tutakuwa na kazi rahisi sana.”