
Taarifa iliyotolewa leo Geneva, Uswisi na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, (OHCHR) inamnukuu Türk akisema kuwa “hii ni mara ya kwanza mashitaka rasmi kuwasilishwa kuhusu utoweshwaji wa watu nchini Bangladesh. Ni wakati wa kihistoria kwa waathirika na familia zao,.”
Wiki iliyopita, Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa ya Bangladesh iliwasilisha mashitaka mawili ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kuhusiana na utekaji na mateso yaliyodaiwa kufanyika katika vituo vya upelelezi vya Kikosi Kazi Maalum Kwa ajili ya Mahojiano na Chumba cha Pamoja cha Mahojiano.
Mahakama hiyo pia ilitoa hati za kukamatwa kwa maafisa wa zamani na walioko jeshini, wakiwemo wakurugenzi wa zamani wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi, pamoja na maafisa wa zamani wa Kikosi Maalum au (RAB).
Jeshi limekamata maafisa
Jeshi la Bangladesh lilitangaza Jumamosi kuwa limewakamata zaidi ya maafisa wake 12 wanaokabiliwa na tuhuma nzito.
Türk amesisitiza kuwa ni muhimu maafisa hao wafikishwe haraka mbele ya mahakama ya kiraia kwa ajili ya kesi kwa haki na uwazi.
“Ninasisitiza umuhimu wa kuheshimu kikamilifu misingi ya haki ya kisheria kama inavyodhaminiwa na sheria za kimataifa. Ulinzi wa waathirika na mashahidi katika kesi hizi nyeti ni lazima uhakikishwe,” amesema.
Mapendekezo ya ripoti yazingatiwe
Türk amekumbusha kuwa ripoti ya Uchunguzi wa Umoja wa Mataifa kuhusu maandamano ya wanafunzi mwaka jana ilitoa mapendekezo makuu ya kuwawajibisha wote waliohusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu – baadhi yakiwa yanaweza kufikia kiwango cha uhalifu wa kimataifa.
Uhalifu wa kutoweshwa sasa unatambuliwa rasmi kisheria nchini Bangladesh baada ya nchi hiyo kuridhia Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Utekaji mwezi Desemba mwaka 2024 na kufanyiwa marekebisho kwa Sheria ya Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa.
Kesi za zamani pia zizingatiwe
Kamishna Mkuu pia ametoa wito kwa mamlaka za Bangladesh kushughulikia kesi nyingine nyingi zilizopo, nyingine zikiwa za zamani na zingine mpya, akisisitiza umuhimu wa mchakato wa haki na kuachiliwa huru kwa wale wote waliokamatwa bila msingi wa kisheria, wakiwemo waathirika wa utekaji, waandishi wa habari na wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa utawala uliopita.
Mchakato wa maridhiano ni muhimu
“Mbali na kuwawajibisha watu binafsi, njia bora kwa Bangladesh ni kuanzisha mchakato wa ukweli, fidia, uponyaji na haki. Mchakato huu lazima ushughulikie historia ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na kuhakikisha haujirudii tena. Na pia naiomba Serikali ya mpito kushughulikia haraka changamoto zinazoendelea kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” amesema Türk.
TAGS: Haki za Binadamu/Asia/Bangladesh/Utoweshwaji/OHCHR