Kwa mujibu wa vyombo vya habari, Odinga amefariki dunia nchini India leo Jumatano tarehe 15 Oktoba 2025 alikokuwa akipatiwa matibabu. Alikuwa na umri wa miaka 80.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia ya hayati Odinga pamoja na serikali na wananchi wa Kenya.

Odinga na uongozi wa kisiasa Afrika

“Odinga alikuwa mtu muhimu katika maendeleo ya kidemokrasia nchini Kenya,” amenukuliwa Guterres, akiongeza kwamba “alikuwa pia mtetezi thabiti wa mageuzi ya kikatiba na utawala jumuishi.”

Katika taarifa hiyo Katibu Mkuu amesema “Odinga atakumbukwa kama mzalendo ambaye mchango wake uliunda taasisi za kidemokrasia nchini Kenya na kuhamasisha uongozi wa kisiasa kote barani Afrika.”

Odinga na Umoja wa Mataifa

Mwaka 2009 akiwa Waziri Mkuu wa Kenya, Odinga alihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambapo pamoja na mambo mengine alieleza kwamba ilikuwa ni “faraja kubwa” kwamba dunia inageukia Umoja wa Mataifa kutafuta njia ya pamoja, ya kimataifa ya kutatua changamoto ngumu zaidi.

“Kulikuwa na wakati ambapo wale wenye nguvu walidhihaki uwezo wa taasisi hii kuwa mchezaji wa kuleta umoja. Hii sasa inabadilika,” alisema Odinga kwenye hotuba yake.

Naye pia wakati huo alipigia chepuo mabadiliko katika Umoja wa Mataifa, hasa upanuzi wa Baraza la Usalama ili kujumuisha viti vya kudumu vyenye haki ya kura turufu kwa nchi za Afrika.

“Dunia haiwezi tena kuendelea kubagua bara ambalo lina zaidi ya watu bilioni moja. Mgogoro wa kiuchumi wa kimataifa pia ulionesha haja ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wenye ufanisi, huku Umoja wa Mataifa ukiwa katikati,” alinukuliwa Odinga.

Mahojiano na Idhaa ya Kiswhili

Na enzi za uhai wake Odinga alizungumza mara kadhaa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa  ikiwemo kuhusu hali ya  Pembe ya Afrika lakini mwaka 2011 alipokuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga alizungumza na Flora Nducha kuhusu Kifo cha Profesa Wangari Maadhai ambapo alisema  “kifo cha mwanamazingira huyo aliyekuwa wa Kimataifa na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ni pigo kubwa kwa Kenya.”

Bi Maathai aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 71 kutokana na ugonjwa wa saratani. Waziri Odinga alisema “Mchango wa Maathai nchini Kenya haupimiki na  atakumbukwa kwanza kama mama wa kwanza ya kufuzu kupata shahada ya digrii katika saikolojia ya elimu. Mama ambaye amechangia zaidi kwa upande wa mageuzi katika nchi yetu. Yaani alikuwa ni mkereketwa katika mstari wa mbele kupigania haki za binadamu katika nchi yetu. Kuona kwamba Wakenya wamejikomboa kutoka kwa utawala wa udikteta ambao ulikuwepo wakati ule. Ameteswa amefungwa, amefanya mambo mengi zaidi na vile vile kwa upande wa mazingira ya hifadhi ya mazingira yetu. Amekuwa kwenye mstari wa mbele kila mara kuona kwamba serikali haikubali kuharibu mazingira kwa kufyeka au kukata misitu yetu. Pia atakumbukwa zaidi katika siku zijazo na taifa letu kama mtu ambaye alikuwa  tayari kulipa gharama yoyote. Kuona kwamba haki ba binadamu na za Wakenya wote zimezingatiwa. “

Pia Wangari Maathai alikuwa mwanamke wa kwanza kutoka barani Afrika kutwaa tuzo ya Amani ya Nobel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *