Chanzo cha picha, Getty Images
Meli ya Titanic labda ndiyo meli maarufu zaidi katika historia, ambayo bado ina msukumo zaidi ya karne moja baada ya kuzama.
Meli ya Titanic ndiyo ilikuwa meli kubwa zaidi ya abiria duniani wakati huo na ilipata umaarufu mkubwa kwa kuzama wakati wa safari yake ya kwanza kutoka Southampton, Uingereza, hadi New York, Marekani, usiku wa Aprili 14 na saa za mapema za Aprili 15, 1912.
Watu 1,500 walipoteza maisha katika janga hili la kusikitisha.
Kuzama kwake kuliendeleza hadithi yake.
Kupitia kutolewa hadharani kwa hati za serikali ya Marekani mnamo 2018, hadithi ya jinsi meli hiyo ilivyogunduliwa sasa iko wazi kwa kila mtu.
Kwa sharti moja
Robert Ballard, ambaye alihusika katika misheni ya siri ya Jeshi la Wanamaji la Marekani, alithubutu kuanza safari ya maisha: kutafuta mabaki ya Titanic.
Ndivyo alivyomwambia Ronald Thuneman, makamu mkuu wa operesheni za Jeshi la Wanamaji.
Jibu la kwanza la Thanman lilikuwa: “Huu ni wazimu mtupu!”
Hata hivyo, Thanman alikubali ombi la Ballard, lakini kwa sharti moja.
Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Wanamaji lingempa rasilimali za kutafuta meli hiyo, lakini ikiwa tu Ballard angetumia rasilimali hiyo hiyo kupata manowari mbili za nyuklia za Marekani ambazo zilizama katika Atlantiki katika miaka ya 1960.
“Nilikubali dau,” Ballard alisema katika mahojiano na CBS au hadithi, “na nikasema, ‘Ikiwa nitafanya kile unachotaka nifanye, unapaswa kuniruhusu kufanya chochote ninachotaka badala yake.”
Misheni hiyo ya siri iliagizwa kibinafsi na Rais wa wakati huo wa Marekani Ronald Reagan, na misheni hiyo ilianza Septemba 1985.
Udhuru wa utafutaji wa Titanic ulikuwa kamili kwa sababu Warusi na vyombo vya habari hawakuwa na shaka kwamba walikuwa wakitafuta manowari zilizozama.
Misheni mbili katika operesheni moja
Chanzo cha picha, Getty Images
Awamu ya kwanza ya misheni ilifanikiwa. Ballard alipata manowari za USS Thresher na USS Scorpion.
Na hatimaye aliweza kutumia muda wake kutafuta Titanic.
Tatizo lilikuwa ni kwamba alibakiwa na siku 12 tu kuipata Titanic kwa sababu boti aliyokuwa akitumia kwa ajili ya shughuli hiyo ingekodishwa na mtu mwingine.
Hatimaye, Ballard aliweza kuipata Titanic katika muda wa siku 8, kutokana na uzoefu alioupata wakati wa kutafuta Scorpion.
“Kulikuwa na watu ambao walikuwa wakimtafuta kwa siku 60, lakini hawakuwa wamempata,” Ballard anasema.
Wachunguzi walipata mabaki ya meli kwenye kina cha kilomita 4 baharini, kilomita 600 kutoka pwani ya Newfoundland, Canada.
Chanzo cha picha, Getty Images
Ballard anakumbuka wakati wa furaha na shangwe alipopata meli hiyo iliozama lakini hisia hizo zilikuwa za kupita.
“Tuligundua kuwa tulikuwa tukicheza na kufurahi juu ya makaburi ya watu ambao walikuwa wamepoteza maisha kwa kuzama, na tuliona aibu,” Ballard anakumbuka.
“Kisha tukawa na utulivu na heshima. Tuliahidiana kwamba hatutachukua chochote kutoka kwa meli hiyo na kwamba tutaiheshimu.”
Wakati huo, wagunduzi wa meli hiyo hawakuwa na nia ya kuiinua meli hiyo wala kuitafuta, lakini katika miaka iliyofuata, mvuto wa meli ya Titanic uliongezeka sana na kusababisha shughuli nyingine za uchunguzi na matokeo ambayo sasa yanaonyeshwa kwenye maonyesho na makumbusho mbalimbali duniani.
Lakini kwa Ballard, ugunduzi wa Titanic pia ulikuwa na ujumbe mwingine wa kusumbua: “Vita vingi baridi vilipiganwa chini ya maji, na Wamarekani hawakujua kamwe kuvihusu.”
Imetafsiriwa na Seif Abdalla