Baada ya kusainiwa kwa mpango wa amani wa vipengele 20 mjini Sharm el-Sheikh, nchini Misri, ambapo mataifa ya Kiarabu na ya Kiislamu yalitia saini, viongozi wa Ulaya walihudhuria lakini hawakushiriki kikamilifu katika mazungumzo. Tony Blair, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, ndiye kiongozi pekee kutoka Ulaya aliyeorodheshwa kwenye “Bodi ya Amani” inayoongozwa na Trump.

Wataalamu wanasema kuwa Umoja wa Ulaya unataka kushiriki zaidi katika kuunda mustakabali wa Gaza na kutatua mgogoro huo.

Je Ulaya itaweza kushiriki zaidi ya kutoa msaada?

Kupitia mtandao wa kijamii wa X, Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ametangaza kuwa umoja huo utatoa ufadhili kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza, ambao unakadiriwa kugharimu zaidi ya dola bilioni 50 na kuahidi kuwa sehemu ya kikundi cha wafadhili wa Palestina.

Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, amesema Umoja Ulaya uko tayari kuchangia katika hatua za mpito za utawala wa Gaza kupitia kamati ya Wapalestina isiyoegemea upande wowote. Pia ameahidi msaada wa kiusalama, sambamba na mpango wa Marekani wa kuunda Kikosi cha Kimataifa cha Kusimamia Usalama (ISF).

Je Ulaya inaweza kupeleka vikosi vyake Gaza

Misri 2025 | Emmanuel Macron
Ufaransa inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa, jambo linalofanya uamuzi kutuma kikosi Gaza kuwa mgumu kwa Rais Emmanuel Macron.Picha: Yoan Valat/Pool via REUTERS

Rais Emmanuel Macron amesema Ufaransa iko tayari kuchangia katika kikosi hicho cha muda, lakini mataifa mengi ya Ulaya bado yanatafakari kabla ya kujitolea. Wataalamu wanasema hali ya kisiasa ya ndani, hasa nchini Ujerumani na Ufaransa, inaweza kuathiri maamuzi hayo.

Jean Loop Samaan, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Mashariki ya Kati ya Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Singapore na mshiriki asiye wa kudumu katika Baraza la Atlantiki, aliambia DW kwamba Ulaya italazimika pia kuzingatia “jukumu ambalo mataifa mengine ya Kiarabu na Kiislamu yanaweza kuchukua katika suala la vikosi vya kijeshi.”

Hata hivyo, kuna sababu za kisiasa za ndani zinazoweza kuathiri maamuzi hayo. Alisema, “Nadhani hili litakuwa suala nyeti sana huko Berlin.” Wakati Ufaransa inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa, jambo linalofanya uamuzi kama huo kuwa mgumu kwa Rais Macron kuuhakikisha.

Hugh Lovatt kutoka Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni amesema Ulaya haitachangia iwapo kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kulazimisha Hamas kujisalimisha kwa nguvu. Badala yake, Ulaya inaweza kuchangia kikosi cha uangalizi kama ilivyofanya kwenye mpaka wa Israel na Lebanon.

Je, Ulaya itajumuishwa Katika Bodi ya Amani ya Trump?

Misri 2025 |
Umoja Ulaya unaendelea kusisitiza suluhisho la mataifa mawili, tofauti na mpango wa Trump.Picha: Mustafa Kamaci/Tur Presidency/Anadolu Agency/IMAGO

Ripoti zinaonyesha kuwa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza — maarufu kama E3— zinapendelea kuwa na mwakilishi katika Bodi ya Amani ya Trump kuhusu Gaza. Hata hivyo, hadi sasa hakuna taifa lolote kati yao lililoalikwa rasmi.

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Rais wa Misri Abdel Fattah el-Sissi kujumuishwa katika bodi ya amani mjumbe wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Steve Witkoff,  alisema “kuna waombaji wengi.”

Hata hivyo Afisa wa zamani wa Israel, ambaye hakutaka kutajwa jina, aliiambia DW kwamba Israel ina mashaka kuhusu uwepo wa wawakilishi kutoka Ufaransa au Uingereza kwenye bodi hiyo, kutokana na hatua yao ya kutambua taifa la Palestina bila makubaliano ya pande zote — jambo ambalo halikupokelewa vyema na Israel.

Lakini hali ni tofauti kwa Italia ambayo inaonekana kuwa na msimamo unaounga mkono zaidi Israel, na hivyo ina nafasi nzuri ya kukubalika kama mshiriki.

Umoja Ulaya unaendelea kusisitiza suluhisho la mataifa mawili, tofauti na mpango wa Trump ambao haujatoa kipaumbele kwa taifa huru la Palestina.

Je, Uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Israel Utaboreka?

Ufaransa Straßburg | Ursula von der Leyen
Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, ametangaza kuwa umoja huo utatoa ufadhili kwa ajili ya ujenzi mpya wa Gaza.Picha: Pascal Bastien/AP Photo/picture alliance

Balozi wa Israel kwa Umoja wa Ulaya, Avi Nir-Feldklein, ameonyesha matumaini ya kuanzishwa upya kwa mahusiano kati ya pande hizo mbili. Katika mahojiano na jarida la Politico Europe, alisema ni wakati wa “kuondokana na hali isiyofurahisha na kurejesha mahusiano mazuri.”

Umoja wa Ulaya ulikuwa umependekeza kusitisha baadhi ya mapendeleo ya kibiashara kwa Israel na kuwekea vikwazo baadhi ya mawaziri wake, ili kuishinikiza nchi hiyo kuongeza misaada na kusitisha opereshi za kijeshi ndani ya Gaza.

Umoja Ulaya hata hivyo umedokeza kuwa kuna uwezekano wa mapitio ya mapendekezo hayo, baada ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini haikutoa uamuzi rasmi.

Ingawa kuna dalili za kurejesha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Umoja Ulaya na Israel, tofauti za kimkakati kuhusu mustakabali wa Palestina bado zipo.

https://www.dw.com/a-74352201

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *