Baraza la Katiba la Cameroon linasema kuwa litatangaza matokeo ya uchaguzi wa rrais siku ya Jumatatu tarehe 27 Oktoba, saa 11 asubuhi kwa saa za huko.

Haya yanajiri baada ya kuhitimisha kusikilizwa kwa kesi jana Alkhamisi.

Majaji walitupilia mbali maombi yote ya ama kufutwa kwa sehemu au uchaguzi wote.

Hivi karibuni Kanisa Katoliki nchini Cameroon liliwataka majaji wa Baraza la Katiba kuhakikisha uamuzi wao unaonesha matakwa ya wapiga kura, likiomba kwamba matokeo yasibadilishwe ili kumpendelea mgombea mwingine.

Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo, miji mikubwa nchini Cameroon imekumbwa na maandamano, huku wengi wakikemea ukiukaji mkubwa wa zoezi la uchaguzi.

Kiongozi wa upinzani na msemaji wa zamani wa serikali Issa Tchiroma Bakary alijitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo na kumtaka Rais Paul Biya akubali kushindwa.

Mamlaka hiyo ilieleza hatua yake hiyo kuwa kinyume cha sheria na kuwataka wananchi kusubiri matokeo rasmi ya Baraza la Katiba.

Akiwa yuko madarakani kwa takribani miaka 43, Paul Biya anawania muhula wa nane wa miaka mingine saba ya kuendelea kubaki madarakani.

Biya mara kwa mara husafiri nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, na mwaka jana uvumi ulienea kwamba alikuwa amefariki dunia, uvumi ambao serikali iliukanusha vikali hadharani.

Nchi hiyo ya Afrika ya Kati inayozalisha kakao na mafuta imekumbwa na changamoto katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kupanda kwa gharama ya chakula, kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kwa vijana, mashambulizi ya silaha kaskazini mwa nchi na mzozo wa kujitenga katika mikoa ya kusini mwa nchi hiyo inayozungumza Kiingereza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *