
Mashabiki wa Galatasaray wa Uturuki wakitangaza himaya na uungaji mkono wao kwa wananchi wa Palestina walipamba majukwaa ya uwanja wa Rams Park kwa bendera ya Palestina na kutoa wito wa kukomeshwa mauaji ya kimbari Gaza.
Tukio hilo lilitokea siku ya Jumatano katika mechi ya Klabu bingwa barani Ulaya kati ya wenyeji Galatasaray ya Uturuki na Bodø/Glim ya Norway. Mashabiki wa Galatasaray waligeuza majukwaa ya uwanja wa Ramses Park mjini Istanbul kuwa rangi za bendera ya Palestina na kuimba nara za kuunga mkono watu wa Gaza.
Mashabiki wa timu ya soka ya Uturuki Galatasaray walinyanyua maelfu ya vipande vya karatasi za rangi ili kutengeneza picha kubwa ya bendera ya Palestina katika sehemu ya kaskazini ya uwanja huo.
Katikati ya onyesho hili la kuvutia, bendera kubwa ya Palestina yenye maneno “Komesha Mauaji ya Kimbari” na nyingine yenye kauli mbiu “Palestina iko Huru” ilijitokeza, na kubadilisha nafasi ya ushindani kuwa eneo la mshikamano wa kibinadamu na malalamiko dhidi ya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Pia, wakati huo huo, kaulimbiu za kuunga mkono Palestina zilisikika kabla na wakati wa mechi, kwa mara nyingine tena zikiwaonyesha mashabiki wa soka kwamba mchezo huu unaweza kuwa sauti ya dhamiri ya ubinadamu, si tu uwanja wa mashindano ya michezo.
Kitendo cha mashabiki wa Galatasaray kilikuwa ni mwendelezo wa utamaduni wa muda mrefu wa mashabiki wa soka wa Uturuki katika kuunga mkono kadhia ya Palestina; utamaduni ambao umerudiwa katika miaka ya nyuma wakati wa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza.
Wachambuzi wa michezo wanasema kilichotokea Istanbul ni dhihirisho la msimamo wa kijamii na kitaifa nchini Uturuki ambao unaenda zaidi ya soka hadi kujitolea kwa maadili kwa haki na ubinadamu.