
Shirika la kimataifa la Oxfam limetangaza kuwa, zaidi ya watu milioni 21 wanahitaji msaada wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hii ikiwa idadi ya karibu humusi moja ya watu.
Taarifa ya shirika hilo imesema kuwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inakabiliwa na mojawapo ya majanga makubwa na yaliyosahaulika ya kibinadamu duniani na kwamba hali inaendelea kuwa mbaya zaidi.
Oxfam, pia imesema unyanyasaji wa kijinsia umefikia viwango vya kutisha, huku mwanamke mmoja akibakwa kila baada ya dakika nne.
Hata hivyo licha ya hali hiyo ya dharura, lakini msaada wa kimataifa unapungua.
Sehemuu nyingine ya taarifa ya Shirika la Oxfam imesema kuwa, katika muda wa mwaka mmoja, ufadhili wa misaada muhimu umepungua kwa thuluthi mbili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na imelitaka kongamano la kimataifa kuhusu Kanda ya Afrika ya Maziwa Makuu, linaotarajiwa kufanyika nchini Ufaransa tarehe 30 mwezi huu wa Oktoba, kuchukua hatua za kivitendo zaidi badala ya matamko na nia.
Wakati huo huo, mapigano makali bado yanaendelea mashariki mwa DRC, licha ya mazungumzo ya kumaliza vita hivyo yanayofanyika Doha kati ya serikali ya DRC na waasi wa AFC/M23.
Pande zote mashariki mwa DRC, yaani waasi wa M23 na wanajeshi wa FARDC, wameendelea kukabiliana huku wote wakituhumiana kwa kuvunja mkataba wa kusitisha vita uliosainiwa mwezi Juni mjini Doha Qatar.
Waasi wa M23 siku ya Alhamisi walituhumu wanajeshi wa serikali kwa kuendelea kushambulia ngome zao ambazo wanazishikilia katika mikoa ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, M23 wakidai hatua hiyo inahujumu mchakato wa amani unaoendelea.
Hata hivyo, Sylvain Ekenge, msemaji wa jeshi la DRC, amekanusha madai ya M23 na kusema, M23 ndio imekuwa ikiyashambulia na wao wamekuwa wakijihami dhidi ya mashambulizi hayo.