Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea wasiwasi wake juu ya kutotumika kwa vituo vingi vya matibabu katika Ukanda wa Gaza, na kutoa mwito wa kufunguliwa tena kwa vivuko vyote kwenye Ukanda huo.

WHO imetangaza kuwa: Tunatoa wito wa kufunguliwa tena kwa vivuko vyote katika Ukanda wa Gaza.

Shirika hilo la afya la kimataifa limeongeza: “Baadhi ya vituo vya matibabu katika Ukanda wa Gaza havifanyi kazi na havifikiki.”

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kwamba, takriban Wapalestina 15,000 wagonjwa na waliojeruhiwa, wakiwemo watoto 4,000, katika Ukanda wa Gaza wanahitaji kutumwa nje ya Ukanda huo ili kuendelea na matibabu na matunzo yao.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Serikali ya Gaza imeripoti kuwa, ni malori 986 pekee ya misaada yaliyoingia katika eneo hilo linalozingirwa tangu kusitishwa kwa mapigano kati ya Harakati ya Mapambano ya Palestina (Hamas) na utawala wa Israel tarehe 10 mwezi huu.

“Ugavi unaendelea kuwa duni baada ya miezi kadhaa ya vizuizi na uharibifu wa makusudi kufuatia vita vya mauaji ya kimbari ya utawala wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza,” imeeleza taarifa ya Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Serikali ya Gaza.

Katika upande mwingine, Philippe Lazzarini, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), amesema kuwa, kurejesha haki ya elimu kwa watoto wa Gaza ni jambo la dharura na muhimu zaidi baada ya kusitishwa mapigano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *