Huku uwezekano wa Marekani kuishambulia Venezuela ukiongezeka, kunajitokeza swali kwamba, je hadithi ya Ghuba ya Nguruwe (Bay of Pigs) itakaririwa kuhusiana na Venezuela?
Rais wa Marekani, Donald Trump, ameamuru kutumwa meli kubwa zaidi ya kubeba ndege za kivina ya USS Gerald R. Ford katika eneo la Caribbean katika kile kinachoonekana kuwa ni kushtadi kile kinachotajwa kama mapambano ya serikali ya Trump dhidi ya “Narco- Terrorism” yaani ugaidi unaohusishwa na biashara ya dawa za kulevya. Kutumwa kwa kundi hilo la ndege za kivita katika eneo hilo kunaweza kuashiria kuanza mashambulizi ya anga dhidi ya shabaha maalumu huko Venezuela. Harakati zilizoshudiwa siku ya Ijumaa zinaashiria kuongezeka uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi kiasi kwamba Pete Hegseth, Waziri wa Vita wa Marekani ameagiza kutumwa katika eneo la Caribbean meli za kivita za kisasa za jeshi la majini la Marekani. Trump pia ameiruhusu CIA kutekeleza oparesheni ya siri huko Venezuela.
Televisheni ya CCN ya Marekani pia imeripoti kuwa Rais Donald Trump anachunguza uwezekano wa kutekeleza mashambulizi katika vituo vinavyodaiwa kuzalisha cocaine na katika njia za kusafirishia madawa ya kulevya ndani ya Venezuela, ingawa bado hajachukua uamuzi wa mwisho kuhusu suala hilo. Itakumbukwa kuwa serikali ya Marekani pia imesitisha mazungumzo na Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro. Venezuela haitambuliwi kama chanzo kikuu cha uzalishaji wa mihadarati aina ya cocaine lakini utawala wa Trump umejaribu sana kumtuhumu Maduro kuwa anaendesha biashara ya dawa za kulevya. Tuhuma hizi zimeelekezwa kwa Maduro katika hali ambayo utawala wa Trump katika miezi ya karibuni umezishambulia boti zisizopungua 10 zinazoshukiwa kusafirisha dawa za kulevya katika pwani ya Venezuela na Colombia ukidai kuwa unapambana dhidi ya magendo ya dawa za kulevya.
Akijibu hatua hiyo ya serikali ya Trump, Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameituhumu Marekani kwa “kuanzisha vita” na kuitaja hatua hiyo kuwa ya uchochezi huko Amerika ya Latini. Matukio haya yote yanaonyesha kuongezeka mivutano kati ya Marekani na Venezuela na kujikita Washington katika kile ilichokitaja kama vitisho vinavyosababishwa na magendo ya dawa za kulevya huko Amerika ya Kusini na Kaskazini.

Swali linaloulizwa ni kwamba, je shambulio lolote la kijeshi la Marekani dhidi ya Venezuela halitakuwa na hatima sawa na mashambulizi ya nchi hiyo katika Ghuba ya Nguruwe?
Mashambulizi yaliyofanywa katika Ghuba ya Nguruwe ni operesheni iliyofeli ya kijeshi iliyofanywa na Marekani Aprili mwaka 1961 ili kupindua serikali ya Fidel Castro huko Cuba. Oparesheni hiyo iliratibwa na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na lengo lake lilikuwa kuwaunga mkono raia wa Cuba wapinzani wa Fidel Castro waliokuwa uhamishoni ili kuishambulia nchi yao na kuipindua serikali ya Kikomonisti ya Fidel Castro ambayo ilikuwa ndiyo kwanza imeasisiwa. Tarehe 17 Aprili mwaka 1961 raia karibu 1,500 wa Cuba waliokuwa uhamishoni waliopewa mafunzo Marekani, waliwasili katika eneo la Ghuba ya Nguruwe kusini mwa Cuba. Hata hivyo oparesheni hiyo ilifeli; kwani wanajeshi wa Cuba wakiongozwa na Castro na kuungwa mkono na wananchi waliweza kutoa kipigo kwa wavamizi katika muda wa siku tatu. Wavamizi zaidi ya 1,200 walitiwa mbaroni na karibu watu 118 waliuawa. Kushindwa huko lilikuwa pigo la kisiasa kwa John F. Kennedy, Rais wa wakati huo wa Marekani, na kulishusha hadhi ya Marekani kimataifa. Aidha, shambulizi hilo liliimarisha nafasi ya Castro huko Cuba na kumuelekeza kuungana pakubwa na Umoja wa Sovieti; hatua ambayo mwishowe ilisababisha Mgogoro wa Makombora wa Cuba mwaka 1962. Kwa mtazamo wa Wacuba, oparesheni hiyo ni nembo ya mapambano dhidi ubeberu wa Marekani na inaadhimishwa kila mwaka ifikapo Aprili 19 kama Siku ya Ushindi. Shambulio dhidi ya Ghuba ya Nguruwe huko Cuba ni mfano wa wazi wa kushindwa uingiliaji kati wa nchi ajinabi mkabala wa irada ya taifa ya nchi ndogo.

Ingawa upo mshabaha kati ya mashambulizi tarajiwa ya Marekani dhidi ya Venezuela na shambulio lililofanywa na nchi hiyo katika Ghuba ya Nguruwe kusini mwa Cuba, lakini inaonekana kuwa ni jambo lililo mbali kukaririwa sinario nyingine kama hii.
Fikra za waliowengi duniani hasa huko Amerika ya Latini hii leo zimekuwa nyeti zaidi kuhusu uingiliaji wa kijeshi wa Marekani, na upo uwezekano wa kutokea upinzani mkali kikanda na kimataifa dhidi ya hujuma za Marekani. Wakati huo huo, Rais wa Colombia, nchi jirani ya Venezuela, Gustavo Petro amebainisha msimamo wake kuhusu uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya Marekani huko Venezuela na kutahadharisha kuhusu hatua hiyo. Brazil pia imetahadharisha kuwa uvamizi wowote wa kijeshi wa Marekani nchini Venezuela utakuwa na madhara makubwa kwa Amerika Kusini yote na utachochea machafuko katika eneo hilo. Kwa maneno mengine ni kuwa, Amerika ya Latini na dunia nzima kwa ujumla inapinga kukaririwa uingiliaji wa Washington katika eneo hilo kwa visingizio visivyo na msingi.