Ripoti iliyotolewa na serikali ya Sudan Kusini kwa ushirikiano na Save the Children imefichua kwamba takriban 64% ya watoto wa Sudan Kusini wenye umri wa kati ya miaka 5 na 17 wanahusika katika aina mbaya zaidi za ajira kwa watoto, ikiwa ni pamoja na ajira ya kulazimishwa, ukatili wa kingono, wizi, na kuhusika katika migogoro ya silaha.
Utafiti wa Kitaifa wa Ajira ya Watoto umechunguza zaidi ya kaya 418 katika majimbo saba na kuonyesha kwamba mgogoro huo umezidishwa na mafuriko yanayoendelea, milipuko ya magonjwa, na migogoro iliyolazimisha mamilioni ya familia kuwa wakimbizi na kuwasukuma kwenye njaa.
Katika wilaya ya kusini mwa Kapoeta, karibu na mpaka na Uganda, watoto 9 kati ya 10 hufanya kazi katika uchimbaji madini, ufugaji na kilimo badala ya kwenda shule.
Viwango kama hivyo vimerekodiwa katika mkoa wa Yambio kusini-magharibi, ambapo migogoro ya kieneo na ndoa za utotoni zimewalazimisha watoto wengi kutumbukia kwenye ajira za utotoni.
10% ya washiriki pia wameripoti kuhusika katika makundi yenye silaha, hasa katika maeneo ya Akobo, Bentiu, na Kapoeta Kusini.
Unyonyaji na dhulma dhidi ya watoto nchini Sudan Kusini hutofautiana kulingana na jinsia zao; aghlabu ya wavulana wanafanyishwa kazi hatarishi au kujiunga na vikundi vyenye silaha, huku wasichana wakikabiliwa na ndoa za kulazimishwa, huduma za nyumbani, na unyanyasaji wa kingono.
“Karibu theluthi mbili ya watoto nchini Sudan Kkusini- na katika baadhi ya maeneo, karibu kila mtoto – anafanya kazi, na suala hili linaashiria mgogoro unaozidi umaskini,” amesema Chris Nyamandi, mkurugenzi wa Save the Children nchini Sudan Kusini.

Ripoti hiyo imesisitiza kwamba elimu ndiyo kinga kubwa zaidi dhidi ya unyonyaji, kwani watoto wanaohudhuria masomo shuleni wana uwezekano mdogo wa kulazimishwa kufanya kazi.