Nabih Berri Spika wa Bunge la Lebanon ametaja uhusiano na umoja uliopo kati ya serikali, wananchi, jeshi na vikosi vya Muqawama kama ufunguo wa kupata ushindi wa mwisho dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Amesema nchi hiyo ya Kiarabu inaheshimu kikamilifu makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa Novemba 2024.

“Tumejitolea kikamilifu  kutekeleza utaratibu uliopitishwa na kamati inayohusika na kufuatilia utekelezaji makubaliano ya kusimamisha vita kwa mujibu wa azimio nambari 1701 linalozijumusha pande zote husika”, amesema Berri katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la kila siku la A Joumhouria.

Azimio nambari 1701 lililopelekea kusitishwa mapigano katika vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Lebanon mwaka wa 2006 linatoa wito kwa utawala ghasibu wa Israel kuheshimu mamlaka ya kujitawala ya Lebanon na haki ya kujilinda nchi hiyo. 

Spika wa Bunge la Lebanon amesisitiza kuwa taifa la Lebanon, serikali, jeshi na Muqawama wanasalia kuwa wachukua maamuzi katika kusambaratisha njama za maadui na kutoa kipigo kwa Israel. 

Baada ya takriban miezi 14 ya vita vilivyokuwa na hasara kubwa na kushindwa kufikia malengo yake katika uvamizi dhidi ya Lebanon, Israel ililazimika kusitisha mapigano na Hezbullah, makubaliano ambayo yalianza kutekelezwa tarehe 27 Novemba mwaka jana.

Tangu wakati huo jeshi la Israel limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya Lebanon, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga na kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *