Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, barua ya pamoja ya hivi karibuni iliyotumwa na Iran, Russia na China kwa Umoja wa Mataifa kupinga jaribio la nchi za Ulaya la kurejesha vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu inaonesha “mshikamano wa kimkakati” uliopo baina ya mataifa hayo matatu yenye nguvu.

Mohammad Baqer Qalibaf ametoa matamshi hayo wakati wa kikao cha wazi cha Bunge hapa mjini Tehran ikiwa ni wiki moja baada ya nchi hizo tatu za Iran, Russia na China kuwaandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama, ikithibitisha kumalizika muda wa Azimio nambari 2231, ambalo liliidhinisha makubaliano ya nyuklia ya 2015 yaliyodharauliwa na kutupwa na Marekani na nchi za Ulaya.

Kwenye sehemu moja ya matamshi yake, Spika Qalibaf amesema: “Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia moja ya mafanikio muhimu na yenye ushawishi katika sera ya kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu, ambayo yametokana na miaka mingi ya Muqawama na ustawi wa wananchi wa Iran licha ya kuweko mashinikizo na vikwazo visivyo vya haki dhidi yetu.”

Amesema, barua hiyo imesainiwa na Wizara za Mambo ya Nje za Iran, Russia na China na hiyo ni ishara ya mshikamano wa kimkakati kati ya mataifa hayo matatu makubwa ambayo yametangaza wazi kwamba njama nchi tatu za Ulaya za kuamsha utaratibu unaoitwa “snapback” kimsingi hazina uhalali wowote wa kisheria.”

Katika barua yao, Iran, Russia na China zilisisitiza kwamba Oktoba 18 inaashiria kufikia mwisho Azimio nambari 2231, na hivyo siku hiyo ndiyo mwisho wa jukumu la Baraza la Usalama la kufuatilia suala la nyuklia la Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *