
Lawrence Wilkerson, kanali msaafu wa jeshi la Marekani ametahadharisha kuhusu hatua yoyote ya Israel ya kuivuta Marekani katika vita na Iran na kusema kuwa Israel inaelewa vyema kwamba itaangamizwa ikiwa itaishambulia Iran bila ya kusaidiwa na upande wowote.
Kanali huyo mstaafu wa jeshi la Marekani ameeleza haya katika mahojiano yake na Jackson Hinkel mchamuzi wa masuala ya kisiasa wa nchini Marekani katika kipindi cha televisheni cha Legitimate Target.
Majadiliano yao yalijikita katika sera za Rais Donald Trump ikiwemo ajenda yake ya sera ya mambo ya nje.
Katika mjadala huo wa televisheni, kanali mstaafu wa jeshi la Marekani ameashiria vita vya siku 12 kati ya Israel na Iran vilivyoanza Juni 13 mwaka huu na kusema Marekani iliingilia kati katika vita hivyo kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran tarehe 22 Juni yaani siku mbili kabla ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita, kufuatia ombi la Israel.
Lawrence Wilkerson amesema kuwa Iran ilijibu mashambulizi ya Israel dhidi ya ardhi yake kwa kuvurumisha makombora ndani ya Israel na kukipiga kituo cha kijeshi cha Marekani huko Qatar.
Kanali mstaafu wa jeshi la Marekani pia amesema: Idadi ya watu waliouawa na kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora ya Iran ilikuwa ndogo kwa sababu Tehran ilijiepusha kushambulia maeneo ya raia.