Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Vahid Jalalzadeh ambaye alielekea Vietnam kwa lengo la kuhudhuria hafla ya utiaji saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni, amehutubia katika hafla hiyo na kusema: Mkataba wa Uhalifu wa Mtandaoni ni hatua muhimu kuelekea upande wa kuanzisha mfumo wa kimataifa wa kupambana na uhalifu wa mtandao na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.

Vahid Jalalzadeh amesema katika hotuba yake hiyo kwamba: Kwa niaba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatoa shukrani zake za dhati kwa serikali na watu wa Vietnam kwa ukarimu wao, heshima na kupangilia vyema tukio hilo la kihistoria la kutia saini Mkataba wa Hanoi.

Jalalzadeh pia ameishukuru sekretariati ya Umoja wa Mataifa kwa mchango wake wa thamani katika kufanikisha mchakato huo. 

Ameeleza kuwa: Kuendelea kwa kasi na kupanuka teknolojia ya habari na mawasiliano kumetoa fursa kubwa kwa maendeleo ya jamii na ubunifu, lakini pia kumeandaa mazingira mapya ya kutokea uhalifu wa mtandaoni, uhalifu unaoruhusu wahusika kuchukua hatua haraka pasina kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

“Jinai hizi zinatishia uhuru wa kitaifa, usalama, uchumi, miundombinu ya mijini na faragha ya watu binafsi duniani kote’ amesema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Ameongeza kuwa, ni muhimu kuwepo ushirikiano wa kimataifa miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. 

Amesisitiza kuwa mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya Uhalifu wa Mtandaoni na hatua muhimu kuelekea kuanzisha mfumo wa kimataifa ya kupambana na uhalifu wa mtandaoni na kuimarisha ushirikiano katika uga wa kimataifa. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa mchango mkubwa katika mazungumzo ya kuandaa Mkataba huo, lengo likiwa ni kuwasilisha mfumo imara na madhubuti wa kisheria kwa jamii ya kimataifa ili kukabiliana na jinai zinazotokana na teknolojia ya habari na mawasiliano, kuwaadhibu wahalifu na kuwalinda watoto na maadili ya umma dhidi ya ongezeko la matumizi mabaya ya teknolojia hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *