
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Watanzania wanatarajiwa kupiga kura, Oktoba 29, kuwachagua madiwani, wabunge na rais, katika uchaguzi ambao rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kushinda.
Rais Samia, mwanasiasa anayezungumza kwa sauti ya upole, alijipata kuwa rais wa kwanza mwanamke, baada ya kifo cha rais John Magufuli mwaka 2021, wakati huo akiwa Makamu wa rais.
Samia mwenye umri wa miaka 65, anatafuta kura, kuweka historia ya kuwa mwanamke wa kwanza, kuchaguliwa katika nafasi hiyo, wakati huu serikali yake inaposhtumiwa kuminya uhuru wa kujieleza na kuwakamata na kuwafunga wapinzani wake kama Tund Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini.
Mwanzoni, alionekana kama kiongozi aliyetaka mageuzi ya kisiasa na maridhiano, kwa kurudisha mikutano ya vyama vya siasa na kuvifungulia vyombo vya Habari vya mitandaoni, vilivyokuwa vimefungiwa wakati wa utawala wa Magufuli.
Hata hivyo, matumaini hayo ya mabadiliko yameyeyuka, baada ya kuanza kushuhudiwa kwa wimbi la wakosoaji wake kutekwa, kukamatwa, kuteswa na hata kuuawa kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty International.
Serilali ya Tanzania, inakanusha ripoti hiyo, na kusema serikali ya rais Samia, haijaacha misingi ya kuheshimu haki za binadamu na ripoti ya Amnesty International haina ukweli.
Kiongozi huyo wa Tanzania, alizaliwa, Januari 27, 1960 visiwani Zanzibar, wakati wa utawala wa Sultan, katka familia ambayo baba yake alikuwa Mwalimu na mama yake, mama wa nyumbani.
Kabla ya kuingia kwenye siasa, aliajiriwa kama karani kwenye ofisi ya serikali huko Zanzibar akiwa na umri wa miaka 17, na baadaye kufanya kazi kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula, WFP.
Mwaka 2000, aliingia kwenye Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama mbunge na kushika nafasi ya Waziri wa serikali ya mitaa, na baadaye akawa Waziri katika Wizara ya ajira, wanawake na watoto.
Mwaka 2010, alichaguliwa kwenye bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, na kuhudumu kama Waziri wa masuala ya muungano wakati wa utawala wa aliyekuwa rais Jakaya Kikwete.
