Dar es Salaam. Bongo ukiachana na viongozi wa serikali na sekta binafsi, wasanii wanaongoza kwa kuwa na walinzi ‘bodyguard’ wanapokwenda katika matukio yanayowakutanisha na nyomi la watu.
Mwananchi linakuchambulia umuhimu wa bodigadi kwa watu maarufu wenye ushawishi mkubwa katika jamii, wanaofanya muziki na filamu.
Aliyewahi kuwa mlinzi wa zamani wa Cristiano Ronaldo staa wa Al-Nassr, Hichman Bukhari alifanya mahojiano namna alivyofanya kazi ya kuhakikisha staa huyo anakuwa salama.
“Vitu vya muhimu kabla ya kutoka, ilikuwa lazima nijue tunapokwenda, aina gani na watu tunaokwenda kukutana nao, kujua njia rahisi za kuingia na kutoka, ili kuhakikisha usalama wake unakuwa mkubwa, kufikiria kwa uharaka, kutatua matatizo na kusalia mtulivu katika hali ngumu.”
Hapa Bongo bodigadi Mudy Mnyama anayemlinda staa wa Bongo Fleva, Harmonize aliwahi kufanya mahojiano na kueleza: “Si kazi rahisi, inahitaji umakini wa kuhakikisha anakuwa salama, kutambua hatari kabla hajadhuriwa na tumekumbana na matukio tofauti ambayo tuliyakabili.”
Bodigadi anatakiwa kufahamu sehemu panapofanyika tukio ili kujua mazingira yote, inapotokea hatari anakuwa anaelewa namna ya kukabiliana nayo na kumuacha mhusika salama.
Iliwahi kutokea Januari 2, 2025 msanii wa muziki kutoka Nigeria, Burnaboy alikuwa jukwaani akitumbuiza katika tamasha lililofanyika Lagos, akavamiwa na shabiki ambaye alikwenda kumbusu miguu yake, lakini staa huyo akamkanyaga kichwani, ndipo walinzi wake wakafika kulinda usalama wake. Japokuwa shabiki huyo alijitokeza mtandaoni na kusema hakuwa na lengo baya yeye ni shabiki yake.
Umuhimu wa bodigadi wanaweza wakaokoa hatari zingine kama ilivyotokea kwa Costa Titch aliyedondoka jukwaani na akakumbwa na umauti.
Desemba 1, 2023 kuna video ilisambaa mtandaoni, ikimwonyesha msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz akiibiwa kofia na shabiki wakati anapita katika umati wa watu Dodoma, huku akimwagiza mmoja wa walinzi wake kuhakikisha inapatikana, hilo ni moja ya matukio yanayoonyesha umuhimu wa kazi hiyo.
Kuna wakati mwingine bodigadi ni mshauri na kuhakikisha ikitokea mwanamuziki ama msanii wa filamu kafanya tukio ama kituko cha aibu, anakuwa anamsaidia kulinda heshima yake kwa kuficha baadhi ya aibu zinazoweza kumshushia heshima mbele ya mashabiki wake.
Inaweza ikatokea msanii kalewa, nguvu ya bodigadi ndiyo inaweza ikaficha hilo kuhakikisha hafanyi vitu vya ovyo ama haongei vitu ambavyo vitachamfua mbele ya jamii.
Ulinzi ni kazi kama zingine, ingawa mara nyingi ni za kujitoa mhanga pia msanii anayekuwa na mabodigadi anamlipa pesa nyingi.
THAMANI KUPANDA
Msanii ambaye anakuwa na mabodigadi thamani yake inakuwa juu, ngumu kufikiwa kirahisi kama ilivyo kwa Diamond, Harmonize, Zuchu, Nandy, Haji Manara msemaji wa zamani wa Simba na Yanga ambaye mara kadha anapotokea katika halaiki ya watu anakuwa na walinzi.
Kuhusu hilo, msanii anayetamba katika tamthilia ya Huba, Julias Charles ‘Giant’ anasema: “Msanii jina lako linapokuwa juu na ukawa na ushawishi mkubwa katika jamii, unaweza ukawa na maadui, kuibiwa hivyo lazima utatafuta watu wa kukusaidia usalama.”
Mwingine ni mwanamuziki mkongwe Juma Nature anasema: “Kuna nyakati kwa watu maarufu kuhitaji ulinzi, maana wakati mashabiki wanataka kupiga picha na wewe huwezi kujua nani mzuri na nani mbaya, hivyo utalazimika kuwa na wasaidizi.”