
Mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Dkt. Ali Akbar Velayati, amesema kuwa Iran, China na Russia, kama mataifa matatu huru yenye nguvu barani Asia, yana nafasi muhimu katika kuunda mfumo mpya wa dunia.
Akizungumza Jumatatu katika kikao na Balozi wa China mjini Tehran, Bw. Cong Peiwu, Dkt. Velayati amesisitiza kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya Iran na China umejengwa juu ya maslahi ya pamoja, heshima ya pande zote, na uhuru wa kisiasa.
Amesifu uhusiano wa “kistratejia na wenye mizizi ya kina” kati ya Tehran na Beijing, akisema kuwa pande zote mbili zina uwezo wa kupanua zaidi ushirikiano wao kwa kuzingatia mabadiliko ya kikanda na ya kimataifa.
Aidha, Velayati ametambua msimamo wa China wa kimsingi kuhusu Iran, hasa katika suala la kile kinachoitwa utaratibu wa “snapback” unaotumiwa na mataifa matatu ya Ulaya kurejesha vikwazo vilivyositishwa kupitia makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, yanayojulikana rasmi kama Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Kwa upande wake, Balozi Cong amesema kuwa uhusiano kati ya China na Iran ni wa muda mrefu na wenye thamani kubwa, na kwamba Beijing daima imeipa umuhimu wa kipekee ajenda ya kupanua ushirikiano wa pande mbili na Tehran.
Ameongeza kuwa China iko tayari kuimarisha zaidi uhusiano huo katika nyanja mbalimbali.
Katika mazungumzo yao, Velayati na Cong walibadilishana maoni kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, yakiwemo upanuzi wa ushawishi wa Marekani na kuingilia kwake masuala ya ndani ya mataifa mengine.
Kwa mujibu wa sera zake za msingi, Iran imeendeleza uhusiano wake na Russia na China katika miaka ya hivi karibuni licha ya vikwazo na mashinikizo makali.
Mnamo Machi 2022, Iran na China zilisaini makubaliano ya kihistoria ya ushirikiano wa kimkakati wa miaka 25, kama njia ya kupinga vikwazo vya upande mmoja vilivyowekwa na Marekani dhidi ya mataifa hayo mawili.
Makubaliano hayo yaliweka rasmi mfumo wa Ushirikiano wa Kimkakati wa Kina kati ya Iran na China, yakifafanua maeneo ya ushirikiano katika siasa, utamaduni, usalama, ulinzi, na masuala ya kikanda na kimataifa.
Vilevile, tarehe 2 Oktoba 2025, Iran na Russia zilianza rasmi kutekeleza Mkataba wa Ushirikiano wa Kimkakati wa Miaka 20, uliotiwa saini na Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na Rais wa Russia Vladimir Putin mjini Moscow mnamo Januari 17, 2025.
Mkataba huo ni hatua muhimu kuelekea kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.