Madrid, Hispania. Nyota wa Real Madrid, Vinicius Junior, anaripotiwa kufikiria kuondoka Santiago Bernabéu baada ya uhusiano wake na kocha Xabi Alonso kufikia hatua ya hatari, kufuatia tukio la kugombana adharani wakati wa El Clásico.

Katika mechi hiyo ambayo Madrid ilishinda 2-1 dhidi ya Barcelona, Vinicius alionyesha hasira kubwa baada ya kutolewa dakika 18 kabla ya mchezo kumalizika. Alionekana kuhoji uamuzi huo mara kadhaa, akisema kwa sauti, “Kwanini mimi kila mara? Basi ni bora niende.”

Kwa mujibu wa gazeti la AS la Hispania, mvutano kati ya wawili hao umekuwa mkubwa kiasi cha kuitwa “mgogoro usioweza kustahimilika”, huku Vinicius akiamini heshima yake imepungua ndani ya timu.

Kwa upande mwingine, uongozi wa Real Madrid unaelezwa kumlinda kocha Alonso, ambaye ameiongoza Los Brancos kukaa kileleni mwa LaLiga kwa tofauti ya pointi tano. Inadaiwa pia kocha huyo ana hasira kubwa na mwenendo wa Vini.

Kwanini Vini amefikia hatua hii?

Msimu huu amemaliza dakika zote 90 mara tatu tu. Mara kadhaa ameanza benchi lakini kwa sasa Mbappe na Bellingham wako katika kiwango bora, hivyo nafasi yake kama mfalme wa Bernabéu inaonekana kuyumba.

Pia ameendelea kukumbana na ubaguzi wa rangi viwanjani nchini Hispania jambo linalomchosha kisaikolojia.

Kwa upande mwingine, Vinicius angependa kusalia Madrid na hata kuongeza mkataba wake unaoisha 2027, iwapo mambo yatatengemaa. Hata hivyo, kwa sasa yupo kwenye mtafaruku wa kihisia na kiusimamizi.

Kile kilichotokea Uwanjani:

Alipotolewa kumpisha Rodrygo katika dakika ya 72 aliuliza kwa mshangao: “Mimi? Kweli?” akaelekea benchi huku akilalamika: “Ni mimi kila mara… afadhali niende tu.”

Akainuka baadaye na kuungana na wachezaji wenzake kana kwamba hakuna kilichotokea. Mwishoni mwa mechi, alihusishwa tena kwenye vurugu ndogo kati ya wachezaji wa timu zote mbili, kabla ya polisi kuingilia kutuliza hali.

Baada ya mchezo, Alonso alizungumzia tukio hilo huku akionekana kutuliza mambo akisema:

“Ni kawaida mchezaji kutaka kuendelea kucheza akihisi yupo kwenye kiwango. Lakini tunatakiwa kufanya maamuzi kwa maslahi ya timu. Tutazungumza, hakuna tatizo lisiloweza kutatuliwa,” amesema Alonso kocha wa Madrid.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *