Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza unaweza kuwa “fursa muhimu” ya kulinda maisha, utu na mahitaji muhimu ya watoto milioni moja wa Kipalestina.

Edouard Beigbeder Mkurugenzi wa UNICEF wa Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ameeleza kuwa, “kusitishwa mapigano huko Gaza kunatoa fursa muhimu kwa maisha, usalama na utu wa watoto, na haipaswi kupoteza fuursa hiyo.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa aliendelea kubainisha kwamba:”Kwa amani, hatua na nia ya pamoja, tunaweza kujenga mustakabali jumuishi na unaozingatia haki kwa watoto wa Gaza.”

Akiashiria kwamba operesheni ya kijeshi ya Israel huko Gaza imesababisha uharibifu mkubwa, amesisitiza kuwa: Maneno na takwimu pekee haziwezi kueleza undani wa maafa haya kwa watoto.

Kwa mujibu wa UNICEF, “Asilimia 85 ya shule za Gaza zimeharibiwa au hazitumiki tena, na shule nyingi zilizobaki zimegeuzwa kuwa makazi ya watu waliokimbia makazi yao; na kujenga upya shule hakuwezekani bila vifaa vya ujenzi.”

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) huko Palestina limeonya kuhusu hali mbaya ya watoto katika Ukanda wa Gaza na kusema: “Kwa mujibu wa takwimu, kwa akali watoto 56,000 wameachwa yatima wakati wa vita, na idadi hii inaongezeka kwa kutisha.”

UNICEF imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba miaka miwili ya milipuko ya mabomu na vita imesababisha uharibifu mkubwa katika Ukanda wa Gaza, na kuua au kujeruhi zaidi ya watoto 64,000. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *