Waziri wa Urithi wa Kitamaduni, Utalii na Sanaa za Mikono wa Iran, Seyyed Reza Salehi Amiri, amesema kuwa utalii ‘Halal’ ni jukwaa muhimu katika kukuza mwingiliano wa kitamaduni na kuwavutia wageni Waislamu.

Salehi Amiri amesema kuwa kuna mpango madhubuti wa kuimarisha ushirikiano wa kiutalii na mataifa jirani pamoja na nchi za Kiislamu. Alisema, “Miongoni mwa malengo yetu makubwa ni kuendeleza utalii na mataifa ya jirani na ulimwengu wa Kiislamu, na katika muktadha huu, utalii ‘Halal’ una nafasi ya kipekee.”

Waziri huyo alibainisha kuwa Iran inatoa kipaumbele kwa Asia ya Kati, eneo la Caucasus na ukanda wa Nowruz, ikifuatiwa na mataifa ya Ghuba ya Uajemi, na baadaye nchi kubwa za Kiislamu kama vile Misri, Indonesia na Malaysia.

Ameitaja chapa ya ‘Halal’ kama mojawapo ya majukwaa yenye mchango mkubwa katika kukuza sekta ya utalii baina ya nchi za Kiislamu, akiongeza kuwa “inaweza kuwa msingi mzuri wa kuwavutia watalii Waislamu kuitembelea Iran na kuongeza mwingiliano wa kitamaduni na kiuchumi baina ya mataifa.”

Akaongeza kuwa, “Kwa bahati nzuri, Iran ni miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele katika nyanja ya utalii Halal na inaendeleza juhudi hizi kwa umakini. Mpango wa pamoja umeandaliwa ili kutangaza uwezo wa kiutalii wa Iran katika nchi za Kiislamu, na mchakato huu utaendelea kwa ushirikiano wa taasisi za kitamaduni na kiuchumi.”

Utalii wa Halal ni sekta inayokua kwa kasi katika safari za kimataifa, ukilenga huduma zinazolingana na maadili ya Kiislamu,  kama vile chakula halali, maeneo ya kuswali, huduma zinazozingatia jinsia, na mazingira yasiyo na pombe.

Kwa mujibu wa toleo la mwaka 2025 la Global Muslim Travel Index (GMTI), idadi ya wasafiri Waislamu wa kimataifa ilifikia milioni 176 mwaka 2024 , ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka 2023, na inatarajiwa kufikia milioni 245 kufikia mwaka 2030.

Utafiti unaonyesha kuwa Iran ilishika nafasi ya 9 miongoni mwa vivutio vyote katika GMTI, na ni miongoni mwa watoa huduma bora za utalii ‘Halal’ kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *