
Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara, ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa mwaka huu, akijihakikishia muhula wa nne madarakani kwa ushindi mkubwa wa asilimia 89.77% ya kura zote.
Hayo ni kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa Jumatatu na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ibrahime Kuibiert-Coulibaly.
Zaidi ya wapiga kura milioni 8.7 walikuwa na sifa ya kushiriki katika uchaguzi huo uliofanyika Jumamosi, ndani ya nchi na katika mataifa ya ughaibuni. Hata hivyo, idadi ya waliojitokeza kupiga kura ilikuwa ya wastani, ikiwa ni asilimia 50.1% pekee.
Katika kinyang’anyiro hicho, wagombea wanne walijitokeza kumpinga Ouattara. Waziri wa zamani wa Biashara, Jean-Louis Billon, aliyempongeza Ouattara siku ya Jumapili, alipata asilimia 3.09% ya kura, huku Simone Gbagbo, aliyekuwa mke wa rais wa zamani, akijizolea asilimia 2.42% tu ya kura zote.
Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa na Baraza la Katiba katika siku chache zijazo.
Mnamo mwaka 2016, Ouattara alifanya mabadiliko ya katiba yaliyofuta kikomo cha mihula ya urais, hatua iliyomruhusu kugombea tena. Katika uchaguzi wa mwaka 2020, alishinda kwa asilimia 94% ya kura .
Hata hivyo, kampeni za uchaguzi wa mwaka huu ziligubikwa na mvutano wa kisiasa, hasa baada ya wagombea wakuu wa upinzani kuzuiwa kushiriki. Hatua hiyo ilisababisha maandamano katika maeneo ya kusini mwa nchi, ambayo ni ngome ya jadi ya upinzani .
Aliyekuwa Rais Laurent Gbagbo, kiongozi wa chama cha upinzani cha African People’s Party of Côte d’Ivoire (PPACI), alizuiwa kugombea kutokana na kupatikana na hatia ya makosa ya jinai, huku Tidjane Thiam, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Credit Suisse, akitupwa nje ya kinyang’anyiro kwa sababu ya kuwa na uraia wa Ufaransa.
Tangu aingie madarakani mwaka 2011, Ouattara amejitambulisha kama kiongozi mwenye dhamira ya dhati ya kuboresha maisha ya vijana. Ameahidi kushughulikia changamoto za kiusalama na kiuchumi zinazolikabili taifa hilo la Afrika Magharibi.
Hata hivyo, viongozi wa upinzani wameendelea kumkosoa kwa kile wanachokiita kushindwa kwake kupunguza pengo la kiuchumi na gharama kubwa ya maisha kwa raia wa kawaida.