Kahama. Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura Kahama Mjini mkoani Shinyanga wamesisitizwa kuwa wazalendo wakati wote wa utekelezaji wa shughuli hiyo.
Wasimamizi hao ni wale wanaokwenda kusimamia vituo vya kupigia kura Kahama Mjini mkoani Shinyanga, katika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika kesho jumatano Oktoba 29, 2025, nchi nzima.
Msimamizi wa uchaguzi Kahama Mjini Sadick Kigaile ametoa rai hiyo jana Oktoba 27,2025 wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa wasimamizi hao.
Amesema ni vyema kila mshiriki akaweka uzalendo mbele wakati wote wa shughuli hiyo ili kuepuka kwenda kinyume na Tume huru ya uchaguzi (INEC).
Amesema “Kuna vituo vipo mbali na ili kufika utakutana na majaruba ya mpunga na mvua hizi unaweza kukuta kuna maji, basi vua viatu pita ufike kituoni, huo ndio uzalendo haswa katika utekelezaji wa shughuli hii muhimu.”
Baadhi ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura Kahama Mjini wakiwa kwenye mafunzo. Picha na Amina Mbwambo
Amewataka kuzingatia viapo vyao, kutunza siri ikiwa ni pamoja na kupunguza matumizi ya makundi sogozi (whatsApp) ili kuepuka kusambaza kwa bahati mbaya nyaraka za uchaguzi ambazo Tume haikutoa maelekezo ya kuzitoa katika utekelezaji wa shughuli hiyo.
“Kiapo cha kutunza siri kipo kwa mujibu wa kanuni namba 8 ya kanuni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na madiwani ya mwaka 2025, ukiukwaji wa kiapo hiki utakuwa umetenda kosa kwa mujibu wa sheria na utawajibika.”Amesema Kigaile na kuongeza
“Ninawaasa kuzingatia muda wa kufungua na kufunga kituo cha kupigia kura, kufanya kazi kwa kushirikiana, kufanya kazi kwa uzalendo na weledi, kuwa na lugha nzuri, kutoa kipaumbele kwa wapiga kura wenye mahitaji maalum wanapofika kituoni na kuhakiki vifaa vya uchaguzi.”
Mwenyekiti wa mafunzo hayo John Makala amemhakikishia msimamizi wa jimbo kuwa washiriki wapo tayari kwenda kutekeleza yale yote yaliyosisitizwa kwenye mafunzo hayo kwa kiwango kikubwa kwa kumtanguliza Mungu.
Amesema “Tahadhari zote ulizozitoa nikuhakikishie kuwa tutaizizingatia ili tuweze kwenda kama timu moja, tunapokwenda katika vituo vyetu tutatekeleza vyote tulivyoelekezwa.”