Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kuipa Pamba Jiji FC pointi tatu na mabao matatu huku Dodoma Jiji FC ikipoteza mchezo tajwa hapo juu kwa kosa la klabu hiyo iliyokuwa mwenyeji kushindwa kuandaa mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hizo kikamilifu, jambo lililosababisha mchezo kuvurugika kisha baadaye kuvunjwa.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 32:1 ya Ligi Kuu kuhusu Kuvuruga

Mchezo huo ambao ulifanyika Jumamosi, Oktoba 25, 2025 katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma, ulilazimika kusimama katika dakika ya sita (6) Dodoma Jiji ikiongoza kwa bao 1-0, baada ya taa za Uwanja wa Jamhuri kuzimika na Dodoma Jiji kushindwa kufanya jitihada zozote za kurejesha mwanga uwanjani hapo ili mchezo uendelee.

“Kutokana na adhabu hiyo na kwa mujibu wa Kanuni ya 32:3 ya Ligi Kuu kuhusu Kuvuruga Mchezo, bao hilo lililofungwa na mchezaji Benno Ngassa wa Dodoma Jiji limefutwa hivyo halitahesabiwa kwenye orodha ya mabao ya mchezaji huyo wala ya klabu ya Dodoma Jiji,” imefafanua taarifa ya TPLB.

Katika hatua nyingine, Mtibwa Sugar imetozwa faini ya Sh20 milioni kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu na kucheza michezo minne (4) ya Ligi Kuu bila kuwa na kocha mkuu mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3(1, 2, 3).

Michezo ambayo Mtibwa Sugar ilicheza bila kuwa na kocha mkuu mwenye ujuzi ni;

M/N 10 – Mashujaa vs Mtibwa Sugar (Septemba 21, 2025)

M/N 19 – Mtibwa Sugar vs Fountain Gate (Septemba 28, 2025)

M/N 28 – Mtibwa Sugar vs Coastal Union (Oktoba 19, 2025)

M/N 36 – Dodoma Jiji vs Mtibwa Sugar (Oktoba 22, 2025)

Adhabu hiyo ya faini Sh5 milioni kwa kila mchezo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Klabu ya TRA United ya mkoani Tabora imetozwa faini ya jumla ya Sh15 milioni kwa kosa la kuanza msimu wa Ligi Kuu na kucheza michezo mitatu (3) ya Ligi Kuu bila kuwa na kocha mkuu mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:3(1, 2, 3).

Michezo ambayo TRA United ilicheza bila kuwa na kocha mku mwenye ujuzi ni;

M/N 9 – TRA United vs Dodoma Jiji (Septemba 20, 2025)

M/N 20 – Pamba Jiji vs TRA United (Septemba 28, 2025)

M/N 34 – TRA United vs Mashujaa FC (Oktoba 22, 2025)

Adhabu hiyo ya faini Sh5 milioni kwa kila mchezo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:19 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

Katika Ligi ya Championship, Kagera Sugar imetozwa faini ya Sh1 milioni kwa kosa la kuchelewa uwanjani katika mchezo wake dhidi ya Barberian.

Daktari wa African Sports ya Tanga, Mohamed Lukuwa amefungiwa michezo mitatu (3) na kutozwa faini ya Sh500,000 kwa kosa la kumshambulia kwa kumpiga ngumi mchezaji wa klabu ya B19, Ramadhani Omary baada ya kutamatika kwa mchezo baina ya timu hizo.

Refa Shomari Lawi kutoka mkoani Kigoma ameondolewa katika ratiba ya waamuzi wa michezo ya Ligi kwa mizunguko mitano (5) kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu katika mchezo baina ya Fountain Gate na Dodoma Jiji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *