Akiwasilisha ripoti ya hivi karibuni kabisa ya Tume ya Uchunguzi, Navi Pillay amesema matokeo hayo yanatokana na uchambuzi wa kisheria uliofanywa chini ya Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu wa Mauaji ya Kimbari.
Amesema “Tumehitimisha kwamba nchi ya Israel inawajibika kwa kutekeleza vitendo vinne vya mauaji ya kimbari Gaza, kwa nia mahsusi ya kuwaangamiza Wapalestina wa Gaza kama kundi”.
Ameongeza kuwa “Tume pia imebaini kwamba Rais, Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi wa zamani wa Israel wamechochea utekelezaji wa mauaji ya kimbari.”
Bi. Pillay, ambaye aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ameelezea hali huko Gaza kama “shambulio la kikatili zaidi, la muda mrefu na pana zaidi dhidi ya watu wa Palestina katika historia.”
Mwanamume akiwa amembeba mtoto mchanga anatembea katikati ya vifusi vya mtaa wake ulioharibiwa huko Gaza.
Uharibifu usioweza kurekebishwa
Amesema kwamba ingawa usalama wa muda na kuachiliwa kwa mateka na wafungwa “vinatoa matumaini, haviwezi kufuta uharibifu uliokwisha kutokea,” akiongeza kwamba “Ukanda wa Gaza sasa umebaki magofu, karibu watu hawawezi kuishi tena.”
Bi. Pillay amesema maafisa wa Israel “wamekuwa wakitangaza hadharani mipango ya kuwahamisha wakazi, kujenga makazi ya walowezi, na kuunganisha maeneo hayo.”
Ingawa usitishaji wa mapigano umezuia utekelezaji wa sera hizo kwa sasa, “matamko ya hivi karibuni ya maafisa wa Israel yanaonesha wazi kwamba malengo hayo bado yapo.”
Hii ni ripoti ya mwisho ya Bi. Pillay kwa Baraza Kuu, baada ya kuongoza chombo hicho cha kimataifa cha uchunguzi tangu Julai 2021.
Ukiukaji katika Ukingo wa Magharibi
Katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, ikiwemo Jerusalemu ya Mashariki, tume ilibaini kuwa sera za Israel tangu Oktoba 2023 pamoja na uungwaji mkono wa wazi na usio wa moja kwa moja kwa walowezi wenye vurugu zinaonesha dhamira ya wazi ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina, kupanua uwepo wa raia wa Kiyahudi wa Israel, na kumeza sehemu kubwa ya Ukingo wa Magharibi.”
Lengo kuu, Bi. Pillay amesema, ni “kuzuia haki yoyote ya Wapalestina ya kujitawala na kuwa na taifa lao, na kudumisha ukaliaji wa muda usiojulikana wa Israeli.”
Wito wa uwajibikaji na haki
Amezitaka nchi Wanachama kuhakikisha haki na uwajibikaji “kwa kusaidia Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC katika uchunguzi wake”, na pia kutumia mamlaka ya kimataifa ya kushitaki washukiwa, wakiwemo wenye uraia wa nchi mbili.
Amesema “Inaniuma kwamba, katika uwasilishaji wangu wa mwisho kama mwenyekiti wa tume hii, mfumo wa kimataifa ulioundwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia umeshindwa kuzuia mauaji haya ya kimbari. Mfumo wa kimataifa umeshindwa kutimiza wajibu wake.”
Amemalizia kwa kutoa wito wa “ukweli na maridhiano,” akisisitiza kwamba “ni kupitia haki ya mpito pekee ndipo amani inaweza kuota mizizi na kustawi.”
Eneo kubwa la Gaza limesambaratishwa na vita
Wito wa usitishaji wa kudumu wa mapigano
Francesca Albanese, mtaalamu huru aliyeteuliwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ardhi za Palestina, pia amewasilisha taarifa kwa kamati ya Baraza Kuu na kusisitiza haja ya usitishaji wa kudumu wa mapigano Gaza.
Ameyataka Mataifa Wanachama kuhakikisha Israel inajiondoa kwenye ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu na kuvunjwa kwa makazi ya walowezi wa Kiyahudi.
Amesema vilevile lazima zisitishe uhusiano wote wa kijeshi, kibiashara na kidiplomasia na Israel hadi itakapositisha na kurekebisha mauaji ya kimbari, ukaliaji haramu na mfumo wa ubaguzi wa rangi .”
Ametaka pia kufanyika kwa uchunguzi na mashitaka, pale inapobidi, kwa wale wanaohusishwa na uhalifu unaodaiwa kufanywa.
“Hivi ndivyo tunavyoanza kuheshimu kumbukumbu za waliouawa,” amesema. “Na ikiwa Baraza la Usalama limekwama, basi Baraza Kuu hili lazima lichukue hatua chini ya azimio la kuungana kwa ajili ya amani, uniting for peace kwa azma kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote.”
Taarifa kuhusu wataalamu huru
Wataalamu huru kama Wawakilishi Maalumu walioteuliwa chini ya utaratibu maalumu wa Baraza la Haki za Binadamu si wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na hawategemei serikali yoyote au shirika lolote. Hawalipwi mshahara kwa kazi yao.