Adnan Abu Hasna, mshauri wa vyombo vya habari wa Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA), amesema kwamba taarifa za hivi karibuni za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambapo alidai shirika hilo la kimataifa halitakuwa na nafasi yoyote katika Ukanda wa Gaza, si jambo jipya na ni katika fremu ya misimamo ya Marekani kuhusu taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Abu Hasna ameelezea kwamba upinzani wa Marekani dhidi ya kazi ya UNRWA ulianza baada ya Donald Trump kushinda muhula wake wa kwanza ambao ulianza Januari 2018, alipopunguza ufadhili wa nchi yake kwa shirika hilo la kimataifa. Baadaye Rais Joe Biden alirejesha ufadhili huo, kabla ya Trump kuamua kuusimamisha tena alipoingia Ikulu mwanzoni mwa mwaka huu.

Abu Hasna amesisitiza kwamba msimamo wa hivi karibuni wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani hauna umuhimu wowote kwa kazi za UNRWA au kutoegemea upande wowote na uwazi wa shirika hilo la kimataifa, hasa ikizingatiwa kwamba Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilitoa uamuzi siku chache zilizopita kwamba UNRWA ni shirika lisiloegemea upande wowote na lenye uwazi linaloheshimu sheria na kanuni za Umoja wa Mataifa, na kwamba halijaingiliwa na makundi ya Wapalestina, kama inavyodaiwa na Israel.

Wanajeshi wa Israel wakizingira ofisi za UNRWA, Gaza

Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilithibitisha Jumatano iliyopita kwamba hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kwamba UNRWA ilikiuka kanuni ya kutoegemea upande wowote au ilifanya ubaguzi katika kusambaza misaada katika maeneo ya Palestina yaliyokaliwa, kama Israel inavyodai mara kwa mara.

Mahakama hilo ilisisitiza kwamba Israel inawajibika kuwezesha utoaji wa misaada kwa watu wa Ukanda wa Gaza, hasa ile inayotolewa na UNRWA.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *